CECIL ODONGO: Wapigakura Luo Nyanza wakatae udikteta wa ODM
NA CECIL ADONGO
HUKU kampeni za uchaguzi mkuu zikiendelea kupamba moto, huu ndio wakati ambapo wakazi wa Luo Nyanza wanafaa kusimama kidete na kukataa udikteta wa ODM.
Hasa wakazi wa kaunti za Siaya na Homa Bay wanafaa kuwakataa viongozi ambao wanalazimishiwa na uongozi wa ODM ambao wamepokezwa tikiti za moja kwa moja.
Kati ya kaunti nne za Luo Nyanza, ni Siaya na Homa Bay ambazo hazijapiga hatua kimaendeleo kwa kuwa magavana wao huwa wamemakinikia kuonyesha utiifu wao kwa Raila Odinga badala ya kuwatekelezea wakazi miradi ya maendeleo.
Wiki jana, ODM ilimpa Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Homa Bay Gladys Wanga tikiti ya Ugavana na duru zinaarifu kuwa Seneta wa Siaya James Orengo na Mbunge wa EALA Dkt Oburu Oginga pia wamepokezwa tikiti ya kuwania Ugavana na Useneta mtawalia katika kaunti ya Siaya.
Hatua hiyo imezua ghadhabu miongoni mwa wafuasi wa ODM katika kaunti hizo ambao baadhi wanadai kuwa viongozi wanaosukumiwa na uongozi wa chama ni wale ambao hawana rekodi yoyote ya maendeleo.
Katika kaunti ya Siaya baadhi ya wakazi wanadai kuwa Bw Orengo ambaye ni wakili maarufu hana rekodi nzuri ya maendeleo kwa muda mrefu ambao amekuwa katika siasa.
Bw Orengo aliingia bungeni kupitia uchaguzi mdogo 1980 kuwakilisha wakazi wa Ugenya.
Alichaguliwa katika chaguzi za 1983, 1988, 1992, 1997, 2007 kama mbunge kabla ya kuchaguliwa tena kama seneta 2013 na 2017.
Kwa karibu miaka 42 ambayo amekuwa katika siasa wananchi wanahoji kuwa eneobunge la Ugenya halikushuhudia maendeleo yoyote ya maana ikilinganishwa na tangu 2013 hadi leo ambapo David Ochieng’ alichaguliwa mbunge.
Bw Orengo sasa hana mpinzani ODM kwa kuwa aliyekuwa mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo na aliyekuwa msemaji wa polisi Charles Owino walihama ODM na kujiunga na UDM baada ya kuhofia kuchezewa shere na uongozi wa Chungwa katika uteuzi.
Dkt Oginga,79 naye anasifika kwa kufanya kazi nzuri akiwa mbunge wa Bondo ila wakazi wengi wanaona kuwa amekuwa na umri mkubwa na anafaa kustaafu siasa.
Ingawa ni haki ya Dkt Oginga kuwania cheo chochote kisiasa, wengi wanahoji kuwa anafaa kumakinikia kampeni za kumsaidia kakake kushinda urais.
Uongozi wa Gavana Cornel Rasanga nao haujanufaisha wakazi wa Siaya mno kutokana na ufisadi uliokolea na kudorora kwa sekta za afya, elimu ya chekechea na nyinginezo.
Mnamo Septemba 2018, DPP aliamrisha Bw Rasanga akamatwe kutokana na ufujaji wa pesa katika kaunti hiyo.
Inadaiwa gavana huyo aliwahi kujigamba kuwa hawezi kunyakwa na vyombo vya uchunguzi kutokana na utiifu wake kwa Bw Odinga.
Kwa kuwa Luo Nyanza ni ngome ya Bw Odinga, wampigie kura za Urais ila za viti vingine wajiamulie badala ya kufuata chama.