Connect with us

General News

Wapigakura wafu 250,000 kutupwa – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wapigakura wafu 250,000 kutupwa – Taifa Leo

Wapigakura wafu 250,000 kutupwa

WALTER MENYA na CECIL ODONGO

MAJINA ya wafu 250,000 yamegunduliwa katika sajili ya wapigakura, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesema.

Kamishna wa IEBC, Justus Nyang’aya, hata hivyo, jana alisema kuwa itakuwa vigumu kuondoa wapigakura wote wafu katika sajili hiyo.

“Tumepokea karibu majina 250,000 kutoka kwa idara inayosajili vifo. Ukweli ni kuwa tutajitahidi sana kuyaondoa majina yao kwenye sajili rasmi lakini si wote kwa sababu watu hufa kila siku hata siku ya uchaguzi wenyewe bado kutakuwa na vifo,” akasema Bw Nyang’aya.

“Hoja muhimu ni kuwa wale ambao wamekufa na majina yao yako kwenye sajili ya wapigakura hawatashiriki uchaguzi huo. Hakuna mfu atakayefufuka kisha kupiga kura,” akaongeza.

Katika chaguzi za awali, idadi ya waliojitokeza kupiga kura katika baadhi ya maeneo huzidi asilimia moja au idadi ya wapigakura waliosajiliwa katika kituo fulani.

Hilo limeibua madai ya kuendelezwa kwa udanganyifu huku hata watu waliofariki wakihesabiwa kama waliopiga kura na kuzua maswali iwapo shughuli hiyo inafanywa kwa uwazi.

Mnamo Machi 1, Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Hussein Marjan alisema kuwa tume hiyo imechelewa kuyaondoa majina ya wafu kwenye sajili ya wapigakura kwa sababu haikuwa imeajiri kampuni ya kufanya ukaguzi na kuyaondoa.

Bw Nyang’aya alisema wananchi watapewa nafasi ya kuthibitisha iwapo wamesajiliwa kuwa wapigakura kati ya Aprili na Mei. Kati ya yale watakayoyathibitisha ni majina, maelezo yaliyonakiliwa kwenye mtambo wa kielektroniki pamoja na kituo cha kupigia kura.

Tayari IEBC imekamilisha mchakato wa utoaji wa tenda kwa kampuni ya KPMG ambayo itakagua majina ya wapigakura kisha kutoa mapendekezo ambayo tume itayatekeleza kabla sajili kupigwa msasa kwa mara ya mwisho.

Kwa mujibu wa Bw Nyang’aya, kutoka mnamo 2018 hadi usajili uliokamilika mnamo Februari, jumla ya wapigakura wapya ambao wamesajiliwa ni milioni 2.7.

Wapigakura wapya 180,938 walisajiliwa kati ya Oktoba 15, 2018 -Agosti 5, 2021. IEBC tena ilikumbatia mchakato mwingine kati ya Oktoba 4-Novemba 5, 2021 na kuwasakili wapigakura wapya 1, 519, 294 huku wengine 421, 057 wakituma ombi kubadilisha vituo vyao vya kupigia kura.

Kati Januari 17- Februari 2022, IEBC iliwasajili wapigakura 1,031, 645 japo ilisema kiwango hicho kilikuwa cha chini mno hasa baada ya idara ya usajili kutangaza kuwa vijana milioni 4.5 walikuwa wapokezwa vitambulisho.

Kamishina huyp alifichua kuwa walilenga kuwasajili kati ya wapigakura 10,000-30,000 kutoka mataifa ya Ughaibuni. Hata hivyo, walifanikiwa kuwasajili 3,538 wapya pekee huku 3, 320 wakituma maombi ya kubadilisha maeneo wanayopigia kura.

“Kuna watu wengi sana ambao walitaka kujisajili ila hawakuwa na vitambulisho. Mahakama pia ilikuwa imeamuru kuwa tuwasajili wale ambao wana kitambulisho pekee lakini tusiwakubali wanaotaka kutumia stakabadhi nyinginezo kama pasipoti,” akasema Bw Nyang’aya.

IEBC inatarajiwa itaanza kutoa mafunzo kwa maafisa wake watakaosimamia uchaguzi mkuu ujao. Maafisa hao watapokezwa mafunzo kuhusu upigaji kura, kuzihesabu na utoaji wa matokeo.

Imebainika IEBC inapanga kuwaajiri kwa muda maafisa 530,000 huku maafisa 10 wakiwemo maafisa wawili wa polisi wakisimamia kila kituo cha upigaji kura.

“Tulikuwa na vituo 44,300 vya upigaji kura mnamo 2017 lakini katika uchaguzi huu idadi hiyo itapanda hadi vituo 53,000,” akasema.