Watatu kufika mbele ya korti kuhusu ajali ya ndege Nakuru 2017
NA JOSEPH OPENDA
MAHAKAMA moja mjini Nakuru imewaagiza watu watatu kufika mbele yake na kutoa ushahidi katika uchunguzi wa umma, kuhusiana na ajali mbaya ya ndege iliyowaua watu watano mnamo 2017.
Hakimu Mkazi Daisy Mose aliwataka mwanapatholojia wa serikali Dkt Titus Ngulungu, mchambuzi Stephen Matunda na Bw Henry Njau watoe ushahidi utakaosaidia katika uchunguzi wa ajali hio.
Ndege hiyo iliyokuwa ikiwasafirisha wanaharakati wanne wa chama cha Jubilee kutoka afisi ya seneta wa Nakuru Susan Kihika, ilitumbukia kwenye Ziwa Nakuru Oktoba 21, 2017 na kuwaua wote waliokuwa safarini.
Rubani wa ndege hiyo, Kapteni Apollo Malowa, Bi Veronicah Muthoni, Bw Anthony Kipyegon, Samuel Gitau na John Ndirangu walipoteza maisha yao kwenye ajali hiyo.
Katika harakati za kuopoa miili ya watano hao, Bw Malowa, Bi Muthoni na Bw Kipyegon walipatikana siku chache baada ya ajali hiyo ila miili ya Mbw Gitau na Ndirangu haikupatikana kabla ya operesheni kuisha.
Baada ya msiba, Kiongozi wa Mashtaka ya Umma aliamuru
uchunguzi wa umma ufanywe Mei 2021 ili kubaini mazingira yanayozunguka ajali hiyo. Kufikia sasa, mashahidi saba wamehojiwa wakiwemo wazazi wa walioaga, walinzi wa Mbuga ya Wanyama ya Nakuru na walioshuhudia mkasa huo.
Kulingana na ripoti ya uchunguzi, rubani wa ndege hiyo ambaye alikuwa Mkuu wa Usalama wa safari za ndege kwenye kampuni ya Flex Air Charters, alifika kwenye hoteli ya Jarika asubuhi ya ajali hiyo, baada ya kuwa nje usiku mzima akijiburudisha.
Ndege hiyo ilitoka saa tisa na dakika 37, japo baada ya ndege kupaa angani, rubani huyo aligeuka na kuelekea upande wa Ziwa Nakuru.
Kampuni ya ndege ilisema haikuelewa sababu kuu ya rubani huyo kupeperusha ndege kuelekea Ziwa Nakuru. Pia haikufahamu iwapo aliamua kufanya hivyo, ili wanne hao wajionee mandhari ya Ziwa Nakuru.
Kulingana na kampuni hiyo, rubani alipaswa tu kusafiri hadi Narok ambayo ni kilomita 42 kutoka Nakuru.
Bi Florence Nyambura (mamake Bw Ndirangu) aliyehojiwa kwanza alisema , alijuzwa habari za tanzia na mpwa wake saa tisa adhuhuri.
Alieleza kuwa alithibitisha habari za kumpoteza kifungua mimba wake baada ya kupigiwa simu na Bi Kihika saa mbili jioni siku iyo hiyo.
Bi Nyambura alieleza kuwa, alikata tamaa ya kuuona mwili wa mwanawe aliyekuwa mwanakampeni mkuu wa Bi Kihika, aliposikia kuwa operesheni ya kutafuta miili kwenye ziwa hilo lilikuwa limefikia ukingoni.
“Shughuli ya kutafuta mwili wa mwanangu ilikuwa imechukua muda mrefu, lakini hakupatikana. Inauma kwa kuwa kila siku nilienda kwenye kingo za Ziwa hilo nikitumai kumpata mwanangu,”alisema Bi Nyambura.
Mwili wa rubani ulipatikana Oktoba 23 mashariki mwa Ziwa Nakuru kilomita nne kutoka eneo ambalo mwili wa kwanza ukigunduliwa.
Kesi hii itaendelea Mei 15.
Next article
Maswali tele kuhusu Kadhi Mkuu kustaafu