Watu walio na kesi wajibwaga siasani
Na CHARLES WASONGA
WASHUKIWA wa wizi wa pesa za umma na uhalifu mwingine wamefurika katika kinyang’anyiro cha kugombea viti mbalimbali kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.
Washukiwa hao wamepata fursa hiyo kutokana na ukosefu wa sheria inayowazima kuwania viti hadi waondolewe mashtaka.
Kufikia sasa zaidi ya wanasiasa 20 ambao wanawania viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 wanakabiliwa na kesi mahakamani kwa tuhuma za kuiba mabilioni ya pesa za umma.
Wanasiasa hao ni kutoka mirengo yote ya kisiasa, hali inayotilia shaka uwezo wa serikali zijazo kupiga vita ufisadi.
Kati ya wanasiasa wakuu walio na kesi mahakamani ni Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, anayekabiliwa na kesi ya wizi wa jumla ya Sh7.5 bilioni.
Wengine mashuhuri ni aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero ambaye ameanza kampeni za kuwania ugavana wa Kaunti ya Homa Bay. Anakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh213 milioni alipokuwa gavana wa Nairobi.
Mbunge wa Lugari, Ayub Savula (Lugari) naye anazongwa na kesi ya uporaji wa Sh122 milioni za Shirika la Kusimamia Matangazo ya Biashara Serikalini (GAA).
Mwenzake wa Malindi, Aisha Jumwa anakabiliwa na tuhuma za wizi wa Sh19 milioni za Hazina ya Ustawi wa Eneo Bunge lake (NG-CDF) pamoja na kesi ya mauaji.
Wanasiasa wengine ambao ni washukiwa lakini wanatetea nyadhifa zao ni Seneta Mithika Linturi (Meru), wabunge James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Alfred Keter (Nandi Hills) na Stanley Muthama (Lamu Magharibi).
Wabunge wengine ni William Kamket (Tiaty) na Johanna Ng’eno (Emurua Dikirr) wanaokabiliwa na kesi za uchochezi wa chuki.
Pia kuna wapya ambao wamejitosa kwenye siasa licha ya kugubikwa na wingu la kesi mahakamani. Hawa ni pamoja na Tabitha Karanja anayetaka kuwania useneta wa Nakuru. Anakabiliwa na kesi ya kampuni yake ya Keroche Breweries kukwepa kulipa ushuru wa Sh14 bilioni.
Naye Bi Lilian Mbogo Omollo, ambaye ametangaza azma ya kuwania useneta wa Embu bado anakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh799 milioni katika Shirika la Vijana kwa Huduma za Taifa (NYS).
Kesi hiyo ingali mahakamani kwani uamuzi kuhusu ombi ambalo Bi Karanja aliwasilisha ya kutaka itupiliwe mbali haijatolewa. Bi Karanja anataka kuwania useneta wa Nakuru kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inasema haiwezi kuwazuia washukiwa kuwania viti kutokana na ukosefu wa sheria za kuiwezesha kuchukua hatua hiyo.
Kulingana na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, vipengele 99 (3) na 193 (3) vya Katiba vinazuia tume hiyo kuwazima washukiwa.
“Mtu hawezi kuzuiwa kushiriki uchaguzi kabla ya rufaa zote za kesi zinazomkabili kusikizwa na kuamuliwa,” akasema Bw Chebukati.
Kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), Twalib Mbarak, ukosefu wa sheria mahsusi hizo ndiyo sababu kuu ambayo imechangia tume hiyo kushindwa kuwazuia wanasiasa wenye kesi.
“Ukosefu wa sheria inayozima kabisa washukiwa wa uhalifu kuwania viti ndio umetufanya kushindwa kuwazuia walio na kesi kushiriki uchaguzi. Katiba nayo inatoa nafasi kwa washukiwa kuwania kabla ya kukamilika kwa kesi dhidi yao,” akasema Bw Mbarak.
Afisa huyo alitoa mfano wa Mbunge wa Bonchari, Pavel Oimeke ambaye mwaka 2021 aliruhusiwa kuwania na akashinda uchaguzi mdogo licha ya kukabiliwa na kesi ambapo ameshtakiwa kuitisha hongo ya Sh200 milioni alipokuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA).
Kulingana na EACC, jumla ya wawaniaji 106 ambao walikuwa na kesi mahakamani waliidhinishwa kuwania viti mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa 2017.
Jaribio la Mbunge wa Ugunja, Opiyo Wandayi kuwasilisha bungeni mswada wa kuwazuia wanasiasa na maafisa wa serikali wenye kesi za ufisadi kuwania nyadhifa katika uchaguzi mkuu liligonga mwamba mwaka jana kutokana na upinzani mkali kutoka kwa wenzake.