– Kando ya visa 309 vipya vya COVID-19, 302 ni Wakenya na wageni saba, wanaume 217 na wanawake 92
– Waziri msaidizi wa Afya Rashid Aman alionya kuwa idadi ya visa nchini vikifikia kilele, vifo pia vitaongezeka huku vituo vya matibabu vikiwa kwenye hatari ya kufurika na wagonjwa.
– Aman alishirikisha kuongezeka kwa maambukizi na wale ambao hukosa kuvalia maski na pia kukiuka sheria za afya
Idadi ya visa vya COVID-19 nchini vimeongezeka hadi 7,886 baada ya watu wengine 309 kupatwa na virusi hivyo Jumapili, Julai 5.
Katibu Mkuu Msaidizi wa Afya(CAS) Rashid Aman alisema wagonjwa hao waligunduliwa baada ya sampuli 4,228 kukaguliwa.
Aman alifichua kuwa ndani ya saa 24, idadi ya waliopata nafuu iliongezeka hadi 2,287 baada ya wagonjwa 51 kuruhusiwa kuenda nyumbani huku walioangamia ikifikia 160 kufuatia kifo cha mgonjwa mmoja.
Katika hotuba yake, Aman alisema huku idadi ya visa nchini vikifikia kilele, vifo pia vitaongezeka huku vituo vya matibabu vikiwa kwenye hatari ya kufurika na wagonjwa.
“Kuongezea kwa idadi ya visa ni maana kuwa watu wengi zaidi watahitaji matibabu na vituo vyetu vitafura. Idadi ya vifo pia inatazamiwa kuongezeka kutokana na hali ya sasa,” alisema Aman
Wagonjwa hao wapya COVID1-19 ni wa kutoka Nairobi (193), Kajiado (22), Kiambu (20), Mombasa (18), Makueni (17), Busia (11), Machakos (tisa), Nakuru (nane) huku Nandi na Turkana vikisajali visa vitatu kila mmoja.
Visa vingine ni kutoka Narok (viwili) huku Kakamega, Nyandarua na Kilifi vikirekodi kisa kimoja.
Kufikia Jumapili jioni, visa vya COVID-19 ulimwenguni vilifikia 11,415,901 ikiwemo 6,463,630 ya waliopona na 534,254 kuangamia tangia kuzuka kwa ugonjwa huo nchini Chini mwishoni mwaka jana.