CHARLES WASONGA: Wawaniaji waeleze jinsi watakavyonasua Wakenya kutoka lindi la mahangaiko
NA CHARLES WASONGA
WANASIASA wanachapa siasa za kujitafutia kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, wawaelezee wananchi peupe jinsi watakavyowaondolea changamoto za kiuchumi.
Baadhi ya watu wameripotiwa kujinyonga kutokana na mzongo wa mawazo unaosababishwa na ukosefu wa pesa za kujikimuVijana wengi waliomaliza masomo ya vyuo vikuu hawana ajira na baadhi yao wamepoteza matumaini maishani.
Wazazi wameshindwa kulipa karo, wengi hawawezi kugharamia mahitaji ya kimsingi kama vile chakula, kodi ya nyumba, maji, umeme miongoni mwa mahitaji mengineyo.
Nakubali kuwa janga la corona na vita vinavyoendelea nchini Ukraine vimeharibu mambo hata zaidi.
Lakini ukweli ni kwamba msingi wa uchumi wetu ulikuwa umeharibika kitambo hata kabla ya janga la corona.
Kwa msingi huo, viongozi ambao watachukua hatamu baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, na wanaosaka kura wakati huu, wafaa kumakinika zaidi na kuelekezea mikakati mipya watakaotumia kuboresha maisha ya Wakenya.
Wagombeaji wakuu wa urais; Naibu Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, waelezee kwa uwazi jinsi mifumo yao ya kiuchumi itaondoa Wakenya kutoka lindi la mahangaiko.
Dkt Ruto aeleze jinsi mfumo wake wa kukuza uchumi kutoka ngazi ya mashinani, maarufu kama “bottom-up” utatekelezwa kwa manufaa ya walalahoi.
Vipi serikali yake itapata Sh100 milioni kila mwaka za kutolewa kwa wafanyabiashara wadogo kama mikopo isiyotozwa riba.
Dkt Ruto aeleze jinsi, fedha hizo zitasimamiwa ili kuzuia uwezekano wa kuibiwa na maafisa wa serikali walafi namna ambavyo fedha za Hazina ya Uwezo ziliporwa.
Kwa upande wake, Bw Odinga aelezee Wakenya jinsi utawala wake utatambua familia masikini hohe hahe na ambazo zitafaidi kutokana na ruzuku ya Sh6,000 kila mwezi.
Bw Odinga pia aelezee Wakenya mbinu mpya atakazotumia kufufua viwanda vikubwa vilivyosambaratika kama vile kampuni ya kutengeneza sukari za Mumias, Nzoia, Miwani, Sony, Muhoroni, Chemilil na kampuni ya Ramisi iliyoko Pwani.
Nadhani Wakenya watapata fursa ya kupata ufafanuzi huu wakati wa mdahalo wa marais utakaoandaliwa na Vyombo vya Habari kati ya Julai 12 na 17 mwaka huu.
Next article
CECIL ODONGO: Mudavadi amejiponza kwa kutogombea kiti…