Connect with us

General News

Wazazi wanaoingiza wana wao sekondari walia kukabiliwa na mahitaji mengi kifedha – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wazazi wanaoingiza wana wao sekondari walia kukabiliwa na mahitaji mengi kifedha – Taifa Leo

Wazazi wanaoingiza wana wao sekondari walia kukabiliwa na mahitaji mengi kifedha

NA BENSON MATHEKA

WAZAZI wanakabiliwa na mzigo mzito huku wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la nane (KCPE) mwaka 2021 wakijiunga na Kidato cha Kwanza kuanzia leo Jumatano.

Mbali na kupanda kwa nauli kutokana na bei ya juu ya mafuta, wazazi wanalalamika kuwa hawakupatiwa muda wa kutosha kujiandaa.

Matokeo ya KCPE yalitangazwa siku 12 zilizopita na wanafunzi wanaojiunga na shule za kitaifa wanaanza kuripoti leo.“Hali ngumu ya kiuchumi inatulemea.

“Muda ambao tulipewa kujiandaa ni mfupi sana lakini tunaelewa ni kwa sababu kalenda ya masomo imebadilika na mwaka huu ni mfupi sana,” akasema Harrison Maina, ambaye mtoto wake aliitwa shule ya kitaifa.

Wazazi walijitahidi ili watoto wao wasikose nafasi katika, shule walizoitwa.

Wengi walisema kwamba bei ya sare na vitabu imepanda sana na wanalazimika kukaza mshipi ili waweze kuwapeleka watoto wao Kidato cha Kwanza.

Baadhi ya shule zimewapa wazazi masharti makali ya kulipa karo kabla ya watoto wao kusajiliwa huku baadhi ya walimu wakuu wakiwataka wazazi kununua sare shuleni kwa bei ya juu.

Kulingana na barua za kuita wanafunzi, shule nyingi zinatoza ada za karo za kati ya Sh6,000 na Sh11,000 za sare.

Wazazi wameomba walimu wakuu kulegeza masharti wakisema kutokana na hali ngumu ya kiuchumi itakuwa vigumu kupata karo yote.

“Walimu wakuu wanafaa kuelewa hali ya kiuchumi inayokabili wazazi wengi ikizingatiwa muda wa kutayarisha wanafunzi ulikuwa mfupi sana,” akasema Anne Mwania ambaye mtoto wake ameitwa shule ya kiwango cha kaunti.

Mwezi Aprili, Waziri wa Elimu Prof George Magoha aliwaambia walimu kutokataa kusajili wanafunzi kujiunga na Kidato cha Kwanza kwa sababu ya kukosa karo.

“Walimu wakuu wanafaa kuwasikiliza wazazi na kukubaliana watakavyolipa karo. Nao wazazi wanafaa kutimiza wanayokubaliana na walimu wakuu,” alisema.

Walimu wakuu wa shule za sekondari wanasema kwamba pesa ambazo serikali inatoa kufadhili elimu ya shule za umma hazitoshi ikizingatiwa gharama ya maisha imekuwa ikiendelea kupanda.

Serikali imekataa ombi la walimu wakuu wa shule za sekondari la kutaka karo iongezwe ili kuwawezesha kuendesha shule.

Walipokutana Mombasa mnamo Aprili kwa kongamano la kila mwaka, walimu hao wakuu walisema kuongezwa kwa karo kungekinga shule dhidi ya mfumko wa bei za bidhaa.