Sekta hii ambayo ndio uti wa mgongo wa ukuaji wa Kenya na Bara Afrika kwa jumla, inaendelea kuhangaishwa na mfumko wa bei ya fatalaiza, mbegu na dawa kukabili wadudu na magonjwa ya mimea.
VAT ya juu inayotozwa bidhaa za kilimo, imetajwa kuwa kiini cha changamoto hizo, Muungano wa Wadau Sekta ya Kibinafsi katika Kilimo (ASNET) ukiirai serikali kuitathmini.
Meneja Mkuu, Agatha Thuo amesema ni kupitia mapunguzo ya ushuru sekta ya kilimo itapata afueni.
Meneja Mkuu, Muungano wa Wadau Sekta ya Kibinafsi katika Kilimo (ASNET), Agatha Thuo akizungumza jijini Nairobi ambapo aliirai serikali kupunguza ushuru unaotozwa pembejeo. PICHA | SAMMY WAWERU
Asnet vilevile, inapendekeza kuondolewa au kufutiliwa mbali kwa VAT ya baadhi ya bidhaa, kama vile mbegu za mboga.
“Tunaiomba serikali ipunguze ushuru unaotozwa pembejeo. Umechangia gharama kuendeleza kilimo kuwa ghali zaidi,” Bi Thuo akasema, akizungumza jijini Nairobi.
“Kama muungano tunasikitishwa na gharama ya juu ya bidhaa za kilimo, hasa fatalaiza.”
Bei ya mbolea imelemea wakulima, licha ya serikali kuzindua mpango wa muda wa fatalaiza ya bei nafuu.
Aidha, Kenya huagiza kutoka nje malighafi yanayotumika kutengeneza fatalaiza na dawa za kilimo.
Russia ndio msambazaji mkuu wa malighafi hayo, na vurugu kati ya nchi hiyo na Ukraine zimechangia kwa kiasi kikuu bei ya pembejeo ulimwenguni kuwa ghali.
Asnet ni muungano mwanabodi wa Chama cha Wamiliki Biashara wa Kibinafsi (Kepsa), na inafanya kazi kwa karibu na serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Ufugaji na Samaki.
“Sekta ya kilimo inachangia thuluthi moja katika ukuaji wa uchumi. Isipuuzwe,” Agatha akasema, akihimiza wadauhusika wengine wa kibinafsi kujiunga na Asnet ili kufanya muungano huo kuwa imara na thabiti.
Kadhalika, Asnet inapendekeza serikali kuongeza mgao wake wa bajeti kwa sekta ya kilimo, kutoka asilimia 2 hadi 10.