Connect with us

General News

2022 ni mwaka wa kila mtu na Mola wake – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

2022 ni mwaka wa kila mtu na Mola wake – Taifa Leo

2022 ni mwaka wa kila mtu na Mola wake

Na LEONARD ONYANGO

HUENDA Wakenya wakapitia hali ngumu zaidi ndani ya miezi 12 ijayo kutokana kupanda kwa gharama ya maisha, sintofahamu katika sekta ya elimu, misukosuko ya kisiasa na jinamizi la janga la corona.

Wadadisi wanaonya kuwa Wakenya wanafaa kujifunga mkanda kupambana na changamoto tele zinazowasubiri.

Elimu

Huku shule zikifunguliwa leo, wazazi wanakabiliwa na hali ngumu ya kutafuta karo na fedha za kununua vifaa vingine vinavyohitajika.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha tayari amewataka wakuu wa shule kuruhusu wanafunzi wasio na karo na sare za shule kuendelea na masomo yao.

“Asilimia 75 ya shule za sekondari ni za kutwa na asilimia 25 ni za bweni. Kwa hivyo, hakuna mwanafunzi anayefaa kubaki nyumbani kwa sababu ya karo huku wenzake wakiwa shuleni,” akaonya Prof Magoha.

Lakini wazazi wamekuwa wakishutumu wakuu wa shule kwa kuwashinikiza kulipa malipo ya ziada na kuwaongezea mzigo zaidi. Mwaka huu, kutakuwa na mitihani mitano ya kitaifa.

Awamu ya kwanza ya mitihani ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) itafanyika kati ya Machi na Aprili.

Wanafunzi ambao sasa wako katika Darasa la Saba na Kidato cha Tatu Julai wataingia Darasa la Nane na Kidato cha Nne mtawalia kabla ya kufanya mitihani yao ya kitaifa Disemba.

Wanafunzi wa Gredi 5 (Darasa la Tano) chini ya Mfumo wa Umilisi (CBC), watajiunga na Gredi 6 Julai na kisha kufanya mtihani wao wa kitaifa Disemba.

Hiyo inamaanisha walimu na wanafunzi watahitajika kujifunga kibwebwe kuhakikisha wanakamilisha silabasi ndani ya miezi mitano.

Siasa

Huku ikisalia miezi saba kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, joto la kisiasa linatarajiwa kupanda nchini huku wanasiasa wakizunguka kila mahali kusaka kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Karibu nusu ya mawaziri – wakiongozwa na Mabw Peter Munya (Kilimo), Eugine Wamalwa (Ulinzi) – wametangaza azma ya kuwania viti vya kisiasa.

Watumishi wote wa serikali wanaomezea viti vya kisiasa, wanatarajiwa kujiuzulu kufikia Februari 9 – hali ambayo huenda ikatatiza huduma.

Uwekezaji

Wataalamu wameonya kuwa joto la kisiasa litafukuza wawekezaji waliolenga kuwekeza nchini.

Bw George Wachira, mkurugenzi wa kampuni ya Petroleum Focus Consultants, anasema Kenya hupoteza asilimia 40 ya muda wa kufanya maendeleo katika mihemko ya kisiasa.

“Shughuli za maendeleo huanza kujikokota takribani miaka miwili kabla ya uchaguzi na miezi kadhaa baada ya uchaguzi. Siasa za mgawanyiko wa kikabila na chuki hushuhudiwa ndani ya kipindi hicho na huathiri pakubwa uchumi kwani wawekezaji wanaogopa kuleta biashara zao nchini,” anasema Bw Wachira.

Madeni

Kiasi cha fedha ambazo Kenya inalipa mikopo kwa mataifa ya kigeni, ikiwemo China, na taasisi za kifedha za humu nchini, kinatarajiwa kuongezeka mwaka huu.

Kenya ilitumia Sh435.7 bilioni kulipa madeni kufikia Juni, mwaka jana. Lakini kuanzia Julai mwaka jana, serikali ilianza kutumia Sh1.023 trilioni kulipa madeni kwa mwaka.

Hiyo inamaanisha kwamba Kenya inatumia Sh2.8 bilioni kulipa madeni kwa siku.Wataalamu wanaonya kuwa kiasi kikubwa cha fedha zinazotumiwa kulipa deni kitasukuma serikali kuongeza ushuru wa bidhaa hivyo kuwa mzigo kwa Wakenya.

Serikali, mwaka huu, inatarajiwa kuendelea na utekelezaji wa masharti makali yaliyotolewa na Shirika la Kifedha la Kimataifa (IMF) kuwezesha Kenya kupata mkopo.

Miongoni mwa masharti hayo ni kupunguza wafanyakazi katika mashirika na taasisi za serikali zinazopata hasara kubwa, ikiwemo baadhi ya vyuo vya umma. Tayari Kenya imepokea mkopo wa Sh109.9 bilioni kutoka kwa IMF.

Corona

Waziri wa Fedha, Ukur Yatani anasema kuwa sintofahamu kuhusu maradhi ya corona ambayo yamelemaza uchumi kote duniani, ingali changamoto.

“Kila uchao aina mpya ya virusi vya corona inagunduliwa. Hali hiyo ni hatari kwa uchumi kwani hatujui hali ya baadaye,” anasema Bw Yatani.