Tumekamilisha fungu moja la mwongo (miaka kumi) na sasa tunaingia katika fungu lingine – elfu mbili na ishirini( 2020).
Tunapoingia katika mwongo mpya ni muhimu kujiuliza umefanya nini ambacho unaweza kukumbuka? Na hili ndilo swali alilouliza babu. Na alipouliza, wajukuu wake walikuwa wamemkodolea macho kwa mshangao mkubwa na hawakutamka lolote.
Mambo yatakayokusaidia kufaulu mwaka huu wa 2020 Source: UGC
Alikuwa mzee mwenye busara nyingi, jina lake Tobias Makali lakini tulimuita Mwendapole, kwa sababu ya upole wake na kila mara alipozungumza, wajukuu wake walimsikiza kwa makini sana. Baada ya muda alianza kuona mabadiliko makubwa katika fikra zao.
Wakati wa Krismasi tulipokutana naye nikiwa na marafiki zangu karibia saba hivi. Alitusimulia visa vingi na jioni hiyo tuliondoka kwake kwenda kulala tu kwani tulikaa naye hadi usiku.
“Wapo wengi wenu ambao mmeoa na kuolewa na mkajaliwa watoto. Lakini kumbukeni kulea mimba si kazi, kazi ni kulea mtoto,” alisema Mwendapole.
Mambo yatakayokusaidia kufaulu mwaka huu wa 2020. Picha: Pinterest Source: UGC
“Sasa katika mwongo huu tuanaonza jiulize ni kipi/lipi ambalo umekuwa nalo tumboni/akilini? Mwongo na mwaka mpya ukianza sasa ni wakati wa vitendo si maneno.” alisema na kutua.
Kisaha akamaliza kwa kusema: “Maneno hayavunji mifupa wala miamba lakini vitendo hufanya.”
Alizungumza kwa muda mrefu na masikio yetu yalimzikiza kwa makini sana wakati akituliwa ndimi za hekima. Alitukumbusha kuwa, ikiwa tulikuwa watu wenye mazoea ya kufanya kitu ambacho hakina natija ni vyema kufikiria tena.
“Wachana nacho. Ikiwa ulikuwa mtu wa kuchagua kazi na kutaka vilivyotayari amka kumekucha. Makosa yote uliyofanya mwaka jana na mwongo jana sahau kumbuka huchelewi kujisahihisha.” Mwendapole alisema huku kikohozi chake kikimfanya kutua kila mara.
Alituambia kuwa, kila mtu hujitengenezea ulimwengu wake. Na kila kitu unachofanya mtu sharti kukifanya vyema. Usifanye vibaya eti kwa sababu si chako. Ikiwa ni kazi, fanya kama yako kwani hujui kesho na ni nani anaona unachofanya. Mungu ndiye mjuzi wa kesho yetu sisi wanadamu.
Vilevile alituomba tusiwe watu wa kujisifu sana na kutukumbusha kuwa, ukinona sana hujikaanga yenyewe.
Mambo yatakayokusaidia kufaulu mwaka huu wa 2020. Picha: 499c Source: UGC
Alichukua dakika chache akiwa kimya na hatimaye akasema: “Wanangu dunia rangi rangile hujui italeta yepi. Jaribu sana kuweka akiba hata kama ni kidogokidogo, churururu si ndo ndo ndo itakufaa siku ya jua. Epuka raha isiyostahili na ishi maisha kutegemea uwezo wako. kumbuka mtu hunyoosha miguu kadiri ya urefu wa kitanda.”
Kisha Mwendapole alisema, ni lazima mtu kujitahidi kwani mwisho wa siku atafaidi, na yeyote hafai kufa moyo.
“Daima mbele. Kumbuka kutenda wema usitaraji malipo wacha Mungu awe ndiye mlifi wako. Nawatakia mwaka na mwongo mpya wenye busara, hekima na baraka tele kutoka kwa mwenyezi Mungu.” alimaliza.
Makala haya yameandikwa na Sakwa Titus mwalimu na mwandishi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsaApp: 0732482690.