MACHI 26, 2021 wakazi wa eneo la Kware, Njiru, Kaunti ya Nairobi waliamshwa na gesi ya vitoa machozi majengo yao yakiangushwa.
Maafisa wa pamoja wa usalama walishika doria, kusimamia matingatinga yaliyogeuza nyumba za kibinafsi na zingine za kukodisha kuwa vifuzi.
Ni shughuli iliyoendelea chini ya ulinzi mkali, kwa muda wa siku kadhaa.
Eunice Wachira, ni mmoja wa wahasiriwa na ambaye nyumba yake ilibomolewa siku iliyofuata, Machi 27.
Mama huyu, pamoja na mume wake walikuwa wamewekeza maelfu ya pesa katika kipande chao cha ardhi, ili kuondokea nyumba za kukodi Nairobi.
“Gharama ya kukodi Nairobi nilikuwa nimeiondokea. Nilijikaza kuboresha nyumba tuliyojenga,” Eunice anasema.
Ni maendeleo yaliyojiri kwa kujinyima.
“Tulikuwa tumechukua mkopo kwenye benki, ambao hadi mkasa wa ubomoaji ulipotukumba hatukuwa tumekamilisha kuulipa,” anaelezea.
Chini ya saa chache, jitihada za wanandoa hao wachanga ziligeuzwa vipande vya saruji, kokoto, mawe na changarawe, visivyo na maana.
Akisimulia, Eunice anasema hakuna chochote cha thamani aliweza kuokoa au kunusuru.
“Niliokoa tangi la maji pekee,” anasema, akikadiria hasara ambayo itamchukua miaka na mikaka kuimarika tena.
Wakati wa ubomozi, wahuni walitumia mwanya huo kunyakua vya wenyewe, maafisa wa vikosi vya pamoja vya askari wakizuia wakazi walioathirika kuokoa wanachomiliki.
Baada ya shughuli hiyo kukamilika, masaveya walitumwa kuweka alama, ishara kuwa waliofurushwa hawatatambulika kamwe.
Licha ya ubomoaji kutekelezwa chini ya ulinzi mkali, serikali ilijiondolea lawama kuhusishwa na umiliki wa ardhi hiyo tata, ikisema: “Ilikuwa oparesheni ya pamoja na inapojiri haina majibu.”
Tetesi nazo zilihoji ardhi hiyo ni ya kibinafsi, baadhi ya maafisa tawala wa serikali eneo hilo wakisema imekuwa na mvutano kwa muda mrefu.
“Mzozo unaoshuhudia haujaanza leo, jana wala juzi, ni wa muda mrefu,” akasema afisa mmoja, aliyeomba kubana jina lake kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari.
Afisa huyo hata hivyo, alihimiza wanunuzi wa ardhi kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kununua.
“Ni muhimu kupitia ofisi ya chifu na viongozi wengine husika wa kata, kaunti ndogo na kaunti, ili kujua historia na uhalisia wa kipande cha ploti au shamba unachonuwia kununua,” akashauri.
Visa vya matapeli wa ardhi si vigeni nchini, hasa katika Kaunti ya Nairobi na viunga vyake, Rais Uhuru Kenyatta akilazimika kuzindua mfumo wa Ardhi Sasa ili kukabili mtandao huo wa wahuni.
Aidha, umeanza kutekelezwa Nairobi, wamiliki wa ardhi, wakitakiwa kusajili upya ploti na mashamba yao.
Hii ina maana kuwa uuzaji na ununuzi utakuwa ukiendeshwa kwa njia ya mtandao, hatimiliki ya kipande cha ardhi ikiwa na mmiliki mmoja pekee, ambaye ni halali.
Rais Kenyatta alisema mpango huo utaenezwa katika maeneo mengine ya nchi, ili kuzima matapeli wa ardhi, na ambao wamesababisha wengi kujuta na hata majeraha na maafa kuripotiwa, kufuatia mizozo ibuka.
Mwanadada Eunice Wachira, mhasiriwa wa ubomoaji wa makazi na majengo eneo la Kware, Njiru, Nairobi, akiwa mtaani Kahawa West. Picha/ Sammy Waweru
Kwa Eunice Wachira na mume wake, David Njuguna, hawana budi ila kusubiri miujuza ya Mungu kutendeka, kuona ikiwa haki itapatikana.
Hata hivyo, mambo yalivyoonekana kutukia wanasema wamesalimu amri, Njuguna akielekea mpakani mwa Kenya na Tanzania, Namanga, kutafutia familia yake changa riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.
“Mume wangu baada pigo la nyumba na mali yetu kuharibiwa, alienda Namanga kusaka kazi. Ni dereva wa matrela, ila vibarua havipatikani kwa urahisi hasa kwa sababu ya athari za janga la Covid-19,” Eunice na ambaye ni mama wa watoto wawili akaambia Taifa Leo kwenye mahojiano ya kipekee majuzi.
Mama huyu anasema amekuwa akitegemea vibarua vya kufulia watu nguo, na si rahisi kuvipata.
Isitoshe, amekuwa na shida za mwili kwa sababu ya baridi, kifunga mimba wake pia akiwa na tatizo la shinikizo la damu.
“Kila wiki, humpeleka kliniki ambayo hugharimu zaidi ya Sh2,000,” akasema.
Pamoja na wanawe, Eunice amekuwa akiishi na shangazi yake, eneo la Kahawa West, Nairobi, ila maisha yanaendelea kuwa magumu, ikizingatiwa kuwa naye pia ana familia.
“Huishi kwenye nyumba ya kukodi, ya mabati. Hutegemea vibarua vya kuchuuza nguo, na kipindi hiki cha corona mambo si mteremko,” Judy Mwihaki, shangazi yake anaelezea.
Eunice Wachira, amelazimika kurejea mashambani, eneo la Kajiado kumtunza mama yake anayeugua.
Ombi lake, akipata msamaria mwema yeyote atakayempa kazi ataridhia, angalau aweze kusukuma gurudumu la maisha.