Firat aita mshambuliaji Dunga aliye na bao moja katika mechi 15 kusaidia Olunga dhidi ya Uganda, Rwanda
Na GEOFFREY ANENE
KOCHA Engin Firat ameamua kumpa nafasi mshambuliaji Ismael Salim Dunga aliyefungia Sagan Tosu bao moja katika mechi 15 za Ligi Kuu ya Japan, katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022.
Stars itapepetana na Uganda Cranes mnamo Novemba 11 ugani St Mary’s Kitende na kukamilisha kampeni yake dhidi ya Amavubi ya Rwanda mnamo Novemba 15 ugani Nyayo katika mechi za mwisho za Kundi E.
Kwa jumla, kocha huyo Mturuki amefanya mabadiliko makubwa kikosi cha Stars kilichobwagwa na Eagles ya Mali kwa jumla ya magoli 6-0 katika mechi mbili zilizopita mwezi Oktoba.
Wengi katika kikosi hicho cha wachezaji 27 hawajachezea Stars kwa muda mrefu ama ni wapya kabisa.
Viungo Johanna Omolo (Kocaelispor, Uturuki), Anthony Akumu (Kaizer Chiefs, Afrika Kusini) na Eric Johanna Omondi (Jonkoping Sodra, Uswidi) wanarejea kikosini pia mabeki Alwyn Tera (Ararat, Armenia), Philemon Otieno (Gor Mahia), Anthony Wambani (Vasalunds, Uswidi) na kiungo Michael Mutinda (KCB).
Dunga amefungia Sagan Tosu bao moja katika michuano 15 tangu ajiunge na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Japan mnamo Januari 25, 2021.
Atashirikiana na mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Japan mwaka 2020 Michael Olunga anayeongoza ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Qatar kwa mabao 10 katika mechi sita, na Masud Juma aliyefungia Difaa El Jadidi goli moja katika michuano minane iliyopita kwenye Ligi Kuu ya Morocco.
Waliotupwa nje kutoka kikosi cha Oktoba ni washambuliaji Henry Meja na Eric Kapaito, viungo Lawrence Juma, Ismael Gonzalez, Eric Zakayo, Phillip Mayaka na mabeki Joash Onyango, David Odhiambo ‘Calabar’, Daniel Sakari, David Ambulu na Farouk Shikalo.
Viungo Wilkins Ochieng (Club Brugge, Ubelgiji) na Timothy Ouma (Nairobi City Stars) wamo mbioni kuchezea Harambee Stars kwa mara ya kwanza kabisa.
Vijana wa kocha Firat wataingia kambini Novemba 6 jijini Nairobi.
Kikosi kizima cha Harambee Stars:
Makipa
Ian Otieno (Zesco, Zambia), Brian Bwire (Tusker), James Saruni (Ulinzi Stars), Gad Mathews (Gor Mahia)
Mabeki
Stanley Okumu (KAA Gent, Ubelgiji), Abud Omar (AEL Larissa, Ugiriki), Eric Ouma (AIK, Uswidi), Bolton Omwenga (Kagera Sugar, Tanzania), Eugene Asike (Tusker), Johnstone Omurwa (Wazito), Philemon Otieno (Gor Mahia)
Viungo
Amos Nondi (Dila Gori, Georgia), Richard Odada (Redstar Belgrade, Serbia), Anthony Wambani (Vasalunds, Uswidi), Kenneth Muguna (Azam, Tanzania), Alwyn Tera (FC Ararat, Armenia), Anthony Akumu (Kaizer Chiefs, Afrika Kusini), Wilkins Ochieng (Club Brugge, Ubelgji), Michael Mutinda (KCB), Duke Abuya (Kenya Police), Timothy Ouma (Nairobi City Stars), Eric Johanna Omondi (Jonkopings, Uswidi), Boniface Muchiri (Tusker), Abdallah Hassan (Bandari)
Washambuliaji
Michael Olunga (Al Duhail, Qatar), Masud Juma (Difaa Hassani El Jadidi, Morocco), Ismael Dunga (Sagan Tosu, Japan)