[ad_1]
TAHARIRI: Mawaziri hawafai kutofautiana hivi
KITENGO CHA UHARIRI
Waziri wa Leba Simon Chelugui amejitokeza kusema kwamba wauguzi wanaotafuta kazi Uingereza hawakufeli mtihani, akitofautiana pakubwa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aliyesema wiki kadhaa zilizopita kwamba kati ya wauguzi 300 waliofanya mtihani wa Kiingereza, ni 10 pekee waliopita.
Kulingana na maelezo ya Bw Chelugui, hatua ya kufanya mtihani huo bado haijafikiwa na kwamba kama wizara inayohusika na ajira, wako mbioni kuwaandaa wauguzi hao kwa ajili ya mtihani huo pamoja na hitaji la vipimo vya kiafya na mtihani wa compyuta.
Aidha, anasema kwamba wauguzi 2,600 wamepita vigezo vya Wizara ya Afya huku akifichua kwamba serikali ya Uingereza imeruhusu uajiri wa hadi wauguzi 20,000.Kufikia wakati tulipokuwa tunaenda mitamboni jana hatukuwa tumepata majibu kutoka kwa Bw Kagwe kuhusu suala hili ambalo sasa linaelekea kuwa tata.
Je, ni nani anayezungumza ukweli kuhusu suala hili na kwa nini kukosa sauti moja katika suala lililo na umuhimu na linaloibua hisia kali kama hili la ufaafu wa wataalamu kwenye kazi zao?Haileti picha nzuri kwa tofauti kama hizi kutokea kwenye serikali haswa wakati kama huu wa siasa za urithi ambapo jambo lolote la aina hii linaweza kuchukuliwa visivyo na madhara yake ni umma kukosa imani na serikali.
Inakumbusha pia nyakati ambazo Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto wametofautiana kuhusu miradi na utendakazi wa serikali. Huku Rais Kenyatta akisema serikali yake imefaulu kutekeleza miradi mingi katika muhula wake wa pili, Bw Ruto amekuwa akikosoa waziwazi na kusema kipindi cha pili ndio kimekuwa duni zaidi katika utendakazi wa Jubilee.
Na huku tofauti hizo za kimaoni zikichukuliwa kuwa kawaida kwa washirika wa kisiasa waliofarakana, umma hautarajii kwamba utafikia hadi kwa “watu wa mkono” kama mawaziri na makatibu ambao uaminifu wao wa kwanza unafaa kuwa kwa kazi waliyopewa kufanyia Wakenya.
Aidha, Rais Kenyatta anafaa aonyeshe udhibiti wa serikali yake kwa sababu mgawanyiko wowote una hatari ya kusambaratisha kumbukumbu kuhusu utawala wake. Miezi michache iliyobakia huenda ikawa muhimu zaidi katika urais wake.
[ad_2]
Source link