[ad_1]
Aston Villa waajiri Steven Gerrard wa Rangers kuwa kocha wao mpya
Na MASHIRIKA
ASTON Villa wamemteua Steven Gerrard kuwa kocha wao mpya kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu ijayo.
Nahodha huyo wa zamani wa Liverpool mwenye umri wa miaka 41 anajiunga na Villa baada ya kuongoza Rangers kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Scotland mnamo 2020-21 kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10.
Gerrard anajaza pengo la kocha Dean Smith aliyetimuliwa na Villa mnamo Novemba 7, 2021 kwa sababu ya matokeo duni yaliyoshuhudia kikosi chake kikipoteza mechi tano mfululizo.
Kufikia sasa, Villa wanashikilia nafasi ya 16 kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 10 sawa na Watford. Ni pengo la pointi tano pekee ndilo linawatenganisha Villa na Norwich wanaovuta mkia kwa alama tano sawa na Newcastle United ambao sasa wananolewa na mkufunzi Eddie Howe aliyemrithi Steve Bruce.
Gerrard alianza kazi ya ukufunzi katika kiwango cha juu akidhibiti mikoba ya Rangers mnamo 2018. Anaagana na kikosi hicho kikijivunia alama nne zaidi kuliko watani wao wakuu Celtic kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Scotland.
Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Villa wamelipa kima cha Sh675 milioni kama fidia kwa ajili ya kuwapokonya Gerrard. Gerrard alichezea Liverpool mara 710 na akaongoza kikosi hicho kutwaa mataji tisa.
Alihamia baadaye nchini Amerika kuvalia jezi za LA Galaxy ya Major League Soccer (MLS) mnamo 2015 kabla ya kustaafu katika ulingo wa soka mwaka uliofuata. Gerrard aliaminiwa kudhibiti mikoba ya chipukizi wa Liverpool katika akademia kabla ya kupewa vijana wasiozidi umri wa miaka 18 kwa ajili ya msimu wa 2017-18.
Sogora huyo ndiye anajivunia rekodi ya kuwajibishwa mara nyingi zaidi katika timu ya taifa ya Uingereza baada ya kuvalia jezi za kikosi hichp mara 114 kimataifa ambapo alipachika wavuni mabao 21. Anajiunga na Villa ambao hawajajizolea alama yoyote kwenye EPL tangu wapepete Manchester United mnamo Septemba 25, 2021.
Kibarua chake cha kwanza kambini mwa Villa ni mechi ya EPL dhidi ya Brighton kabla ya waajiri wake kumenyana na Manchester City, Liverpool na Chelsea kwa usanjari huo kabla ya mwisho wa mwaka wa 2021.
[ad_2]
Source link