Kangemi PAG FC Safina ya kuwakomboa vijana maovuni, kukuza na kuinua talanta kwa weledi
Na PATRICK KILAVUKA
ILIKUWA mara ya kwanza kwa Kangemi PAG FC ya Kangemi, kaunti ya ndogo Westlands kushiriki Ligi ya Shirikisho la Soka Kenya FKF, Kaunti -ndogo, tawi la Nairobi West na kuibuka ya pili bora nyuma ya DESAI FC alama (27) na (25) mtawalia.
Ilibuniwa 2017. Wachezaji walioanzisha walikuwa wa kanisa la Kangemi PAG. Lakini walipanua mawazo kushirikisha vijana wengine kuingia na safina kama njia ya kuwakomboa vijana maovuni, kukuza na kuinua talanta. Usimamizi mzuri wa kocha Wilson Otieno (alikuwa mchezaji wa timu kabla kuchukua usukani), kinara Vincent Season, katibu Desmond Kasese na mwekahazina Emma Lufuta, umeipandisha ngazi ya kupepetana katika Ligi ya Kaunti, FKF, Nairobi West, 2021-2022.
Inajitegemea, Ina wachezaji 32 ambao wanapigia zoezi na kucheza michuano ya ligi uga wa Kihumbuini. Kocha Otieno anasema timu imekuwa moto wa pasi kutokana na uwiano mwema ambao umekumbatiwa na wanasoka pamoja na wadau. Mtangasuano wao, umeitia timu joto na motisha zaidi hata wakati huu wa maandalizi ya ligi kwani imekomoa au kutoshana nguvu na timu za ligi ya hadhi kama Leads United 0-0 (Ligi ya Kitaifa Daraja ya Pili), Red Carpet 1-1 (FKF, Kanda, Nairobi West ), Kangemi Allstars 3-0 (Kitaifa Daraja ya Kwanza) na Kangemi Atletico 2-1( FKF, Kauntindogo).
Mkufunzi huyo anasema wanao mwito kwamba, bidii na ujasiri ni nguzo ya kusonga mbele! Wanazamia kuendeleza kampeni hadi Ligi ya Supaligi (NSL) Hata hivyo, changamoto kuu ni ufadhili,vifaa vya mazoezi vya kutoshana na uhisani. Ingawa hivyo, wanaamini hatua kwa hatua watafikia azma.
Ushauri kwa wizara ya michezo ni kwamba, inafaa kuyapa kipa umbele masuala ya mchezo mashinani kwa kuzisaidia timu ili, ziwape wachezaji fursa ya kuonyesha vipaji katika majukwaa mbalimbali ya soka. Ikiwezekana timu ambazo zinashiriki ligi mbalimbali zitembelewe kuona kimasomaso changamoto zinazopitia.
Kikosi cha Kangemi PAG kutoka Kangemi kikicheza dhidi ya Kangemi Atletico uwanjani Kihumbuni .PICHA/PATRICK KILAVUKA
Mafanikio yake ni kwamba tayari imepandishwa ngazi ya Ligi ya Kaunti na itaipiga kwa ukucha kwa jino.