TAHARIRI: Kenya ina kila sababu kujali hali ya majirani
Na MHARIRI
KENYA ina sababu nyingi za kushughulikia changamoto zinazokumba mataifa jirani.
Kwa muda sasa, mataifa jirani ya Ethiopia na Uganda yamekumbwa na misukosuko ya kisiasa na changamoto zingine za kiusalama.
Nchini Ethiopia, kundi la waasi limetishia kupindua serikali.
Wakati mwingi mapinduzi ya serikali husababisha migogoro ambayo hutatiza usalama wa nchi.
Hali hii huweza kuzorotesha usalama wa nchi zinazopakana na ile iliyofanyiwa mapinduzi ya utawala, hasa katika hali ambapo mapinduzi hayo husababisha vita vinavyodumu kwa miaka mingi.
Nchini Uganda, milipuko ambayo imekuwa ikitokea katika siku za hivi majuzi ni matukio ya kutisha.
Milipuko hiyo inayohusishwa na mashambulio ya ugaidi inatokea wakati asasi za kiusalama za Kenya pia zimekaa chonjo ikiaminika kuna habari za kijasusi kuhusu uwezekano wa mashambulio nchini.
Kando na tishio la kiusalama katika taifa hili, matukio hayo katika nchi jirani hutishia pia hali ya uchumi wa Kenya.
Hii ni kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Kenya na majirani wake kibiashara.Mashirika mbalimbali yaliyo na makao yao makuu nchini yamewekeza biashara za mabilioni ya pesa katika nchi jirani.
Hivyo basi, mandhari ya kibiashara yanapovurugwa katika nchi hizo, Kenya itapata pigo kwa mapato yanayotokana na ushuru ambao makampuni hayo hutozwa.
Kando na hayo, kuna wananchi wengi wa Kenya ambao huwa wameajiriwa katika mataifa hayo au wanaendeleza biashara zao.
Hawa ni wananchi ambao wengi wao hutegemewa kurudisha kiasi cha mapato yao kwa uwekezaji mwingine nchini, au kusaidia jamaa zao walio Kenya kimaisha.
Jukumu la serikali ni kulinda maslahi ya wananchi wake wote, iwe wanaishi nchini au nje.
Hivyo basi, jambo lolote linaloweza kutishia maisha na biashara zao popote walipo linafaa kuchukuliwa kwa uzito.
Kenya hunufaika pia kwa kuwa eneo ambalo linategemewa kupitisha abiria na bidhaa wanaoelekea kwingine, kupitia baadhi ya nchi jirani.
Kuna ndege za mashirika ya kimataifa ambayo huenda yakasitisha au kupunguza safari zao zinazopitia humu nchini endapo hakutakuwa na usalama katika mataifa jirani.
Hilo litakuwa pigo la kiuchumi kwa nchi hii.Nchi nyingi jirani hutegemea Bandari ya Mombasa kuagiza mizigo kutoka nchi za nje, ambayo baadaye husafirishwa kwa barabara au reli.
Next article
Ulimi wa Ruto wamweka hali mbaya Mlimani