TAHARIRI: Tushabihiane na hadhi yetu katika riadha
Na MHARIRI
SI siri kuwa Kenya ni taifa linaloogopwa sana katika michezo ya riadha hasa fani ya mbio.
Ni taifa ambalo mataifa mengine yanaposikia likitajwa, huingiwa na mchecheto kwa ubabe wake.
Si katika mbio za mita 800, 1,500m, 3000m kuruka viunzi na maji, 5,000m, 10,000m, marathon, mbio za nyika na hivi majuzi zaidi mbio za mita 100, zote Kenya ni jitu la kuogopwa.
Ni taifa lenye usemi mkubwa katika spoti hii kiasi cha siku za hivi majuzi, raia wake kuanza kupewa vyeo mbalimbali katika uongozi wa shirikisho la riadha duniani (World Athletics).
Nani ajuaye, labda siku zijazo Mkenya ndiye atakayeongoza shirikisho hilo maarufu duniani!
Hilo linapofanyika, serikali na wadau katika riadha hawaonekani kuchangamkia fursa zinazojitokeza za kuvuna kutokana na umaarufu huo.
Kuna njia mbalimbali ambazo tunaweza kutumia kupata utajiri wa kigeni.
Miongoni mwa njia hizo ni kuzidisha juhudi za kujipigia debe katika medani ya kimataifa kama taifa murwa la kunoa vipawa vya riadha na kujiandaa kwa mashindano mbalimbali ya kiwango cha kiulimwengu na barani.
Njia nyingine ya kutumia kuvuna kutokana na fursa hii ni kuhakikisha kuwa tunawaandaa wanamichezo wetu vyema kwa kutumia miundomsingi ya hadhi ya kisasa.
Aidha, sharti tuwafunze wakimbiaji wetu, hasa waliobebea, kupigania fursa za kutumiwa kwenye kuvumisha bidhaa za kampuni mbalimbali za kimataifa.
Mojawapo ya udhaifu wa Kenya katika ulingo wa kimataifa umekuwa kukosa kuwatayarisha wakimbiaji wake hasa kisaikolojia na kimawasiliano.
Kutokana na hilo utawakuta wakimbiaji wa Kenya wametia fora sana katika mbio fulani lakini kutokana na udhaifu wa mawasiliano wanahofia ama hawavutii mashirika yenye nia ya kuwatumia kama mabalozi wa bidhaa zao.
Hiyo ina maana kuwa tunahitaji kuwaandaa wakimbiaji wetu katika fani ya mawasiliano na kujiamini ili waweze kuvuna kutokana na nafasi nomi za kibiashara zisizohusiana na mbio moja kwa moja.
Naam, wapo Wakenya kadhaa, japo wachache wanaotumiwa na kampuni kadhaa za kimataifa kuvumisha bidhaa zao akiwemo Eliud Kipchoge, bingwa wa marathon.
Hata hivyo, kampuni za humu nchini zinafaa kuhimizwa kuwatumia zaidi wakimbiaji wetu kujivumisha.
Vilevile, Serikali inafaa ihakikishe kuwa hivi karibuni inavutia shirikisho la riadha kukubali kuipa Kenya ruhusa ya kuandaa mojawapo ya mashindano ya kimataifa kama vile Riadha za Dunia au Jumuiya ya Madola, si za chipukizi tu.
Bahati mbaya hilo halitawezekana bila miundomsingi mizuri. Kwa hivyo uimarishaji wa miundomsingi utakuwa muhimu zaidi.