[ad_1]
Wapiganaji wapora chakula cha msaada
Na MASHIRIKA
SHIRIKA la Chakula Duniani (WFP) limesimamisha usambazaji wa misaada ya chakula katika miji miwili kaskazini mwa Ethiopia, baada ya watu waliojihami kuvamia maghala yake na kuiba chakula kilichokuwepo.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa (UN), vikosi vya Tigray vilivamia maghala hayo katika mji wa Kombolcha.Walitishia kuwashambulia wafanyakazi wake, ikiwa wangewazuia kuchukua chakula hicho. UN ilisema watu hao waliiba misaada mingi, hata ile iliyopangiwa kuwasaidia watoto wanaokumbwa na utapiamlo.
Eneo hilo linakumbwa na baa la njaa kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya wapiganaji wa Tigray na vikosi vya serikali.UN inasema zaidi ya watu milioni tisa wanakumbwa na njaa kutokana na mapigano hayo, ambayo yamedumu kwa mwaka mmoja.
Msemaji wa WFP nchini Ethiopia alisema, wafanyakazi wake “walitishiwa vikali wakati wa uvamizi huo.” Akaeleza: “Hatutakubali vitisho kama hivyo kutekelezwa dhidi ya wafanyakazi wetu. Ni vitisho vinavyoathiri pakubwa juhudi za UN na washirika wake kutoa misaada hiyo wakati na mahali inakohitajika.
” WFP pia ilivilaumu vikosi vya serikali dhidi ya kutumia nguvu kutwaa malori yake matatu na kuyatumia kwa shughuli zake. Hatua hiyo ndiyo inayotajwa kuchangia shirika hilo kusimamisha shughuli za usambazaji chakula katika miji ya Kombolcha na Dessie.
Miji hiyo ni baadhi ya maeneo muhimu yanayotumika na UN kwa shughuli zake katika eneo la Amhara.Vikosi vya Tigray havijatoa taarifa yoyote kuhusiana na madai hayo. Majuzi, serikali ya Ethiopia ilitangaza imetwaa miji hiyo kutoka kwa wapiganaji hao.
Hata hivyo, wapiganaji hao walisema wanajeshi walitwaa tu maeneo ambayo walikuwa wameondoka.Mapigano yalitokea katika eneo hilo mwaka mmoja uliopita kati ya serikali na wapiganaji wa chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF), ambacho kimekuwa kikidhibiti siasa za Ethiopia kwa muda mrefu.
Next article
Mvurya aeleza sababu za kuunga naibu wake
[ad_2]
Source link