TAHARIRI: Mafuriko: Mikakati ya kuzuia hasara ibuniwe
Na MHARIRI
SERIKALI ya kitaifa pamoja na za kaunti zinatakikana kujitahidi kupunguza au hata kuzuia hasara zinazotokea kila mara msimu wa mvua unapoanza baada ya ukame.
Kwa wiki chache sasa, taifa limeshuhudia uharibifu wa mali baada ya mvua kubwa kunyesha katika sehemu mbalimbali za nchi huku pia vifo vikianza kuripotiwa.
Mbali na vifo vya wananchi, miongoni mwa hasara zilizotokea ni maafa ya mifugo, mashamba yaliyokuwa yametayarishwa kwa kilimo, na miundomsingi kama vile barabara na madaraja.
Haya yote yametokea mara moja baada ya msimu wa kiangazi ambao ulidumu kwa muda mrefu.
Wakati wote wa kiangazi, hasara zile zile ambazo zinashuhudiwa wakati huu wa mvua pia zilitokea.
Inahofiwa kuna watu waliofariki kwa sababu ya athari za makali ya njaa, maelfu ya mifugo wakaangamia na mimea ikanyauka mashambani.
Ni aibu kuwa kila mwaka, lazima serikali ikumbushwe kuhusu wajibu wake wa kuepusha maafa na hasara zinazotokana kwa njia hiyo.
Wakati mwingi serikali huzungumzia juhudi zilizowekwa kuwezesha uzalishaji wa chakula kwa njia za kisasa ikiwemo unyunyuziaji maji mashambani.
Lakini ukame unapotokea, inadhihirika kuwa miradi inayotangazwa mara kwa mara bado haisaidii wananchi.
Isitoshe, kuna miradi mingi inayosemekana inaendelezwa ya kujenga mabwawa katika sehemu mbalimbali za nchi ila huenda inatekelezwa mwendo wa kinyonga kwani wananchi wengi bado huteseka kwa kiu.
Matatizo haya yote yanapoendelea, maji ambayo yangehifadhiwa ili yatumiwe katika unyunyizaji mashambani au kujaza mabwawa huwa yanaendelea kuangamiza binadamu badala yake.
Ni sharti suala hili lichukuliwe kwa uzito kwani linahusu maisha ya wananchi.
Haifai nchi iwe ikijivunia kuhusu mambo kama vile ukuaji wa uchumi, ustawishaji miundomsingi na teknolojia wakati ambapo raia wake wanateseka kwa mambo ambayo yanaweza kutatuliwa haraka.
Haya ni mambo ambayo yalifaa kutatuliwa miaka mingi iliyopita punde baada ya taifa kupata uhuru kutoka kwa wakoloni.
Tatizo ni kuwa, tumekosa nia kutoka kwa viongozi wetu kwa miaka hiyo yote ndiposa kipaumbele huenda kwa miradi ambayo mwananchi haoni faida.
Wakati huu ambapo nchi inajiandaa kwa Uchaguzu Mkuu mwaka ujao 2022, ni vyema wananchi wawe makini kuhusu ahadi ambazo wanasiasa watawatolea.