Wakazi wa Nairobi kukosa maji siku mbili, leo na kesho
Na HILARY KIMUYU
BAADHI ya wakazi wa Nairobi huenda watakosa maji kati ya siku ya Jumanne na Jumatano wiki hii kutokana na kufungwa kwa Kiwanda cha Maji cha Ngethu.
Kampuni ya Maji na Majitaka mjini Nairobi (NCWSC) mnamo Jumatatu ilitangaza kufungwa kwa kiwanda hicho ili kuwezesha kuunganishwa kwa bomba jipya la Kiambu na Embakasi kwenye bomba la Ngethu Gigiri katika Bwawa la Kiambu ili kuwezesha usambazaji wa maji katika maeneo ya Embakasi, Mihango, Utawala na Ruai mradi huo utakapokamilikam Juni 2022.
“Hii itarahisisha kuunganishwa kwa bomba jipya la Kiambu na Embakasi kwa bomba la Ngethu katika bwawa la Kiambu,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Nairobi Water, Nahashon Muguna.
Baadhi ya taasisi na kampuni zitakazoathirika kutokana na operesheni hiyo ni Chuo Kikuu cha Nairobi Bewa Kuu, Kiwanda cha Coca Cola, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, EPZ-Athi river na eneo la Mlolongo.
Maeneo mengine yatakayoathirika ni yale yanayopatikana karibu au kando ya barabara kama vile Langata, Kibra, James Gichuru road, riverside, Westlands, Lavington, Kilimani na Kileleshwa.
Hata hivyo, wakazi watakaoathiriwa wanaombwa kuwa watulivu kwani mradi huo hautachukua muda.
“Tunawaomba wateja wetu wawe watulivu na pia tunawahimiza kutumia maji yanayopatikana kwa uangalifu tunapoendelea na mradi huo,” akasema Bw Muguna.
Mwaka huu pekee, wakazi wengi wa mji wa Nairobi wamelazimika kustahimili ukosefu wa maji kutoka kampuni za kusambaza maji mnamo Februari, Mei, Juni, Julai na Septemba kutokana na mradi unaoendelea wa uboreshaji wa miundombinu.
Nairobi imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa maji tangu Aprili 2017 na kuwalazimu wakazi wengi kugeukia maji kutoka kwenye visima au yale yanayotolewa kwa bei ghali na wachuuzi wa maji.
Takriban asilimia 50 pekee ya wakazi wa Nairobi wanapata maji ya moja kwa moja ya bomba huku waliosalia wanategemea maji kutoka kwa vioski, wachuuzi, viunganishi visivyo halali au kutoka kwa visima.
hata hivyo, wale wanaopata maji ya bomba moja kwa moja, ni asilimia 40 tu ya eneo hili hupokea maji kwa masaa 24 kwa siku na iliyobaki kupata maji kwa wastani wa masaa 11.
Next article
Lempurkel hatimaye huru kutoka jela