Aussems asema Leopards haitatoboa msimu huu
Na CECIL ODONGO
MKUFUNZI wa AFC Leopards Patrick Aussems amewakorofisha nyongo mashabiki wa timu hiyo baada ya kusema wazi kuwa timu hiyo haiwezi kushinda ligi kutokana na ukosefu wa wanasoka wazoefu.
Leopards ambao wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara 13 wamekuwa na msimu mgumu. Baada ya kujibwaga uwanjani mara 10, Ingwe imeshinda mbili, ikasajili sare mara tatu na ikapoteza mara tano; ikiwa imejikusanyia alama tisa na inashikilia nafasi ya 15 kati ya timu 16.
Aussems, 56 anasema kuwa matokeo haya yamechangiwa na ukosefu wa wachezaji wazoefu baada ya kambi yake kuhepwa na waliokuwa wachezaji mahiri kutokana na njaa.
“Hatukutarajia tungeshiriki ligi na timu hii inayojivunia wachezaji wachanga. Nilitarajiwa kuwa ningekuwa na wachezaji wangu tegemeo msimu jana ila karibu wote wakahamia timu nyingine,” akasema Mbelgiji huyo.
“Hiki kikosi hakiwezi kutwaa taji la ligi au kutoa ushindani kwa timu nyingine. Kampeni yetu haitakuwa rahisi ila lazima wajitahidi na tupate matokeo ambayo yatatuweza kusalia ligini,” akaongeza Aussems.
Hata hivyo, Aussems anasisitiza kuwa wanasoka hao huenda wakang’aa zaidi msimu ujao kwa kuwa watakuwa wamepata tajriba ya kutosha kwenye kampeni ya sasa.
“Uzoefu utakuja kutokana na mechi hizo ambazo tunacheza dhidi ya baadhi timu zenye wanasoka mahiri na waliocheza kwa miaka mingi.
La muhimu ni kuwa wanaendelea kujifunza na baada ya miezi michache, hali yao itakuwa imeimarika,” akasema.
Kati ya wachezaji waliogura Leopards ni aliyekuwa nahodha Isaac Kipyegon, Elvis Rupia, Robinson Kamura, Hansel Ochieng, Austin Odhiambo, Fabrice Mugheni Bienventure Shaka, Boniface Wafula na Cylide Senejaji. Wengine Jaffer Owiti, Sellasie Otieno, Harrisson Mwendwa, Ezekiel Owade na Said Tsuma.
Ushindi pekee wa Leopards ni 1-0 dhidi ya Tusker katika mechi ya ufunguzi mnamo Septemba 26 na matokeo sawa na hiyo dhidi ya Posta Rangers mnamo Disemba 9.
Next article
Omicron: Safari 6,000 za ndege zafutiliwa mbali