Connect with us

General News

Juhudi za Duale na wenzake kuyeyusha malengo ya mswada wa vyama zafeli bungeni – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Juhudi za Duale na wenzake kuyeyusha malengo ya mswada wa vyama zafeli bungeni – Taifa Leo

Juhudi za Duale na wenzake kuyeyusha malengo ya mswada wa vyama zafeli bungeni

Na CHARLES WASONGA

JUHUDI za Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale za kuifanyia marekebisho sehemu ya tano ya Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Kisiasa ili kuondoa hitaji la vyama hivyo kuwa na sera na itikadi madhubuti zimefeli bungeni.

Hii ni baada ya jumla ya wabunge 150 wa mrengo wa handisheki kupiga kura ya kudumishwa kwa hitaji hilo huku wabunge 136 wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wakipiga kura ya kutaka liondolewe.

Bunge la kitaifa lilikuwa limekutana kwa kikao maalum Jumatano, Desemba 29, 2021 kwa ajili ya kukamilisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Kisiasa katika hatua ya tatu na ya mwisho.

Duale alitaka sehemu hiyo iondolewe ili watu wanaotaka kusajili chama cha kisiasa wasitakiwe kuandamanisha taarifa kuhusu sera na itikadi za chama hicho kwenye maombi kwa afisi ya Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa.

Pendekezo lake liliungwa mkono na wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto na ambao wanaegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Lakini wabunge wanaounga mkono handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wakiongozwa na kiongozi wa wengi Amos Kimunya walipinga kuondolewa kwa hitaji hilo wakisema kutachangia kuchipuza kwa vyama vidogovidogo “visivyo na maana yoyote” almaarufu, brief case parties.

“Matokeo ya upigaji kura kuhusu mabadiliko yaliyopendekezwa na Bw Duale ni kama ifuatavyo; upande wa NDIO umepata kura 136 na upande wa LA umepata kura 150. Matokeo hayo yanaashiria kuwa mabadiliko ya Bw Duale yameshindwa,” akasema mwenyekiti wa kikao Chris Omulele (Mbunge wa Luanda).

Kuangushwa kwa marekebisho hayo yaliyopendekezwa na Bw Duale kulimaanisha kuwa marekebisho sawa na hayo yaliyopendekezwa na wabunge Didmus Barasa (Kimilili) na John Mutunga (Tigania Magharibi) pia iliangushwa.

Hata hivyo, majira ya asubuhI mrengo wa Rais Kenyatta na Bw Odinga alipata pigo baada ya wandani wa Dkt Ruto kushinda katika raundi ya kwanza ya kuyeyusha mswada huo unaoruhusu miungano ya vyama kuchukuliwa kama vyama vya kisiasa.

Hii ni baada ya pendekezo la Mbunge wa Tigania Magharibi Bw Mutunga kwamba vyama viwe na rangi kuu, kando na alama kupitishwa kwa kura 123 dhidi ya 118 za upande uliopinga.

Bw Mutunga alitaka sehemu ya 3 ya mswada huo ifanyiwe marekebisho ili rangi kuu (dominant colour) pia itumiwe kutambua chama cha kisiasa. Pia alitaka suala la usawa lizingatiwe wakati wa usajili wa vyama vya kisiasa.

Kupitishwa kwa pendekezo hilo kuliashiria kuwa mrengo wa Tangatanga ulishinda katika juhudi zake za kutaka rangi kuu pia itumiwe kutambua chama cha kisiasa.

Lakini juhudi za wandani wa Naibu Rais Dkt Ruto za kupunguza mamlaka ya Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kwa kupendekeza kubuniwe kwa Bodi maalum ya kusimamia shughuli za vyama vya kisiasa zilikataliwa na Naibu Spika Moses Cheboi.

Bw Cheboi alisema kuwa pendekezo hilo lililowasilishwa na wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Owen Baya (Kilifi Kaskazini) na John Kiarie (Dagoretti Kusini) lingebadilisha malengo ya mswada huo.

“Marekebisho yaliyopendekezwa na Ichungwa, Baya na Kiarie yangebadili dhima na malengo ya mswada huu na hivyo yanapaswa kuwasilishwa kwa umma kwa ukusanyaji wa maoni. Kwa hivyo, marekebisho ambayo yanafafana yamekataliwa,” akasema Bw Cheboi.