Connect with us

General News

Uunganishaji haramu wa stima waweka wakazi gizani miezi 12 – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Uunganishaji haramu wa stima waweka wakazi gizani miezi 12 – Taifa Leo

MAKALA MAALUM: Uunganishaji haramu wa stima waweka wakazi gizani miezi 12

Na SAMMY KIMATU

WAKAZI katika mitaa kadhaa ya mashariki mwa kaunti ya Nairobi hasa ya mabanda eneo la Mukuru, wanazidi kuhangaika wakikaa gizani mwaka mmoja baada ya kampuni ya Kenya Power kuondoa transfoma eneo hilo kwa kuhangaishwa na matapeli.

Wafanyakazi wa kampuni hiyo ya kusambaza stima wakishirikana na maafisa wa polisi waliojihami kwa bunduki walifanya msururu wa misako katika mitaa hiyo lengo lao likiwa watu wanaounganishia stima kiholela na kinyume cha sheria.

Misako iliendeshwa kuanzia mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kwa Njenga ulioko kwenye kaunti ndogo ya Embakasi Kusini, Mukuru-Kwa Reuben ulioko kwenye kaunti hiyo,Mukuru-Sinai, Mukuru-Paradise, Mukuru-Jamaica, Mukuru-Lunga Lunga na Mukuru-Doonholm iliyoko kaunti ndogo ya Makadara.

Msako uliendelea hadi mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kingstone, Mukuru-Tetra Pak ambayo imo katika kaunti ndogo ya Makadara. Katika mtaa wa Mukuru-Kwa Njenga, wananchi walizua rabsha kujaribu kutibua shughuli ya kung’oa transfoma kutoka mtaani.

Kwa wakati mmoja, maafisa wa KP walilazimika kubomoa ukuta wa simiti uliofunikia nyaya zilizokuwa na nguvu nyingi ya stima zilizotumiwa na matapeli kusambazia wakazi stima kinyume cha sheria.

Matapeli hao walikuwa wakiunganishia stima wakazi na kuwatoza ada ya kati ya Sh500 na Sh1,000 kulingana na mahitaji.

“Ikiwa utawekewa stima kwa nyumba, walitoza Sh500 kwa kila mwezi. Ikiwa stima yako itawekwa saluni au duka iliyo na jokovu, ulilazimika kuwalipa Sh1,000 kwa mwezi,” alisema mkazi mmoja wa mtaa wa Mukuru Kayaba.

Kampuni hiyo hupata hasara kufuatia hatua ya matapeli kuunganisha stima kinyume cha sheria na kuhatarisha wakazi na mali yao..

“Wanaoiba stima ni matajiri wakubwa ikizingatiwa kuwa hakuna ushuru hutozwa kwao wala hakuna peni inaingia kwa serikali. Kampuni huripoti hasara ya mamilioni ya pesa kufuatia kuharibika kwa transfoma zilizolipuka baada ya kubebeshwa moto kupita kiasi,’’kampuni inasema kwenye ripoti.

Takriban transfoma zaidi ya 20 ziliondolewa mitaani na kubebwa wakati wa msako huo.

Kulingana na afisa mmoja wa polisi asiyeruhusiwa kutoa habari kwa wanahabari kwa mujibu wa itifaki, matapeli walikuwa wakiunganisha stima jioni hata baada ya msako na ndio sababu kampuni iliamua kubeba transfoma.

Alitoa mfano wa tukio moja mtaani Lunga Lunga, wanaume walipounganisha nyaya za stima kutoka kwa nyanya zinazosambaza stima ndani ya kampuni.

“Tulipoondoka mtaani Mukuru-Lunga Lunga, nyakati za usiku, wanaume walijiunganishia stima katika laini zinazoingia ndani ya kampuni eneo la Viwanda na mtaa ukarudi katika hali yake ya kawaida,” afisa huyo alielezea Taifa Leo.

Katika barabara ya Entreprise, transfoma iliyokuwa ndani ya kampuni moja iliondolewa baada ya kudaiwa ilisambaza stima mtaani jirani wa Mukuru-Maasai.

Katika steji ya Kayaba kulikokuwa na transfoma iliyosambaza stima mtaani Mukuru-Kaiyaba, mamia ya wakazi walitokea kwa wingi walipopata habari transfoma inaondolewa.

Giza totoro ilizagaa kuanzia siku hiyo hadi leo na hakuna dalili ya transfoma kurudishwa hivi karibuni.

Transfoma nyingine zilizoondolea ni pamoja na iliyokuwa mkabala wa barabara ya Sigei, karibu na eneo la Lengo mtaani Mukuru-Kayaba.

Nyingine iliondolewa kutoka mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina baada ya kulipuka na wakazi kuchota mafuta yake.

Kutoka Mukuru-Paradise hadi Mukuru-Kaiyaba, transfoma zaidi ya kumi ziliondolewa.

“Baada ya mtaa wa Kayaba kukosa stima, walisambaziwa stima kutoka kwa trasnfoma ya mtaa jirani wa Mukuru-Hazina ndiposa kutokana na kubebeshwa sana, ililipuka na haijawai kurudishwa tangu wahandisi wa KPLC walipoibeba,” Bw David Kiarie, mwenyekiti wa usalama mtaani humo alisema.

Misako zaidi iliendeshwa katika mtaa wa Mukuru-Sokoni, Mukuru-Kenya Wine, Mukuru-Commercial, Mukuru-Kisii, Mukuru-Kaberira na Mukuru-Shimo-La Tewa, Mukuru-Fuata Nyayo na Mukuru-Mariguini.

Mkuu wa tarafa ya South B, Bw Michael Aswani Were alisema serikali ilifanya misako hiyo ili ikomeshe sakata ya wizi wa stima ikinuia kupatia wananchi stima safi, salama na ya bei nafuu.

“Serikali inanuia kupatia wananchi stima salama na yenye bei nafuu mitaani badala ya maisha yao kuhatarishwa na wanaojiunganishia stima kiholela. Tumepoteza maisha ya watu kadhaa kupitia wizi wa stima,” Bw Were asema.

Kando na hayo, miaka mitatu iliyopita, Benki ya Dunia ilizindua mradi wa kuweka stima katika mitaa ya mabanda ya Mukuru.

Hata hivyo, milingoti ya stima na nyaya ziliwekwa mitaani lakini mradi wenyewe ulikwama.

Leo, kinachoonekana mitaani ni milingoti bila nyaya na mita zake.

Matumaini yameanza kuonekana katika mtaa wa Mukuru-Kwa Reuben, ambapo stima imerudishwa kupitia mradi wa serikali wa kuunganisha wakazi stima wa Last Mile.

“Wakazi wana stima wanayolipia, kuna maji safi, barabara za lami na mitaro ya kupitisha maji machafu,” mwakilishi wa wadi eneo hilo, Bw Evans Otiso alisema.

Wakazi katika mitaa isiyo na stima wanaomba serikali kuwasaidia wakisema wanapata hasara kubwa hasa wafanyabiashara wanaolazimika kufunga kazi zao mapema wakihofia usalama.