Mchujo tishio jipya la kusambaratisha UDA
Na WANDERI KAMAU
HUENDA ndoto ya Naibu Rais William Ruto kujenga chama chake cha UDA kuwa cha kitaifa ikavurugika, kutokanana tashwishi ambazo zimeanza kuibuka kuhusu ikiwa shughuli ya mchujo itaendeshwa kwa njia ya wazi.
Tayari, baadhi ya wanasiasa waliokuwa wandani wa Dkt Ruto wameanza kuonyesha dalili za kugura chama hicho, licha ya kukipigia debe hapo awali.
Ingawa wengi hawajajitokeza wazi, hofu ya kuwepo mapendeleo kwenye shughuli ya uteuzi mwaka huu 2022 ndiyo inayotajwa kuchangia tashwishi hizo.
Kufikia sasa, Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Kirinyaga, Bi Wangui Ngirichi, ndiye mwanasiasa aliyejitokeza wazi kueleza kutoridhishwa kwake na jinsi uongozi mkuu wa chama unaendesha baadhi ya shughuli zake.
Alhamisi, Bi Ngirichi alitangaza kuhama chama hicho na kuanza harakati za kupigania ugavana katika Kaunti ya Kirinyaga mwaka ujao kivyake.
“Nilikuwa mmoja wa watu waliojenga UDA kifedha na hata kuivumisha katika Kaunti ya Kirinyaga na eneo la Mlima Kenya kwa jumla. Hata hivyo, kwa sasa nataka kuangazia kampeni yangu ya kuwania ugavana pekee. Wenyeji wa Kirinyaga wako huru kumchagua mwaniaji urais wanayependa—iwe ni Dkt Ruto au kiongozi wa ODM, Raila Odinga. Nitaendesha kampeni zangu kivyangu,” akasema Bi Ngirichi.
Mbunge huyo alisema asingeendelea kuwa katika mrengo wa kisiasa ambapo kuna njama zinaendeshwa kwa njia fiche kuwapendelea watu fulani.
Ingawa ghadhabu ya Bi Ngirichi imetajwa kuchangiwa na hatua ya Gavana Anne Waiguru kuhamia UDA, imebainika kwamba si Kirinyaga pekee ambako mivutano hiyo inashuhudiwa.
Duru zinaeleza kuwa mivutano sawia inaendelea katika kaunti za Nyandarua, Nakuru, Murang’a, Kilifi, Uasin Gishu kati ya nyingine.
Katika Kaunti ya Nyandarua, baadhi ya wagombea wanaolenga kuwania ugavana kwa tiketi ya UDA wamekuwa wakilalamika kwamba tiketi ya chama tayari ishapewa mbunge Faith Gitau, anayelenga kuwania nafasi hiyo pia.
Katika Kaunti ya Nakuru, kumekuwa na malalamishi ya chini kwa chini kuwa Seneta Susan Kihika ashapewa tiketi ya UDA.
Bi Kihika ametangaza kwamba atawania ugavana.
Katika Kaunti ya Murang’a, baadhi ya wawaniaji wa ugavana wametishia kuhama chama hicho baada ya madai kuibuka kwamba Seneta Irung’u Kang’ata ashapewa tiketi.
Hali ni iyo hiyo katika Kaunti ya Kilifi, ambapo wawaniaji kadhaa wamejitokeza kudai mbunge Aisha Jumwa (Malindi) atapendelewa kwenye shughuli ya mchujo kutafuta atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye kinyang’anyiro cha ugavana.
Katika Kaunti ya Uasin-Gishu, wawaniaji wanalalamika kuwa mbunge Caleb Kositany (Soy) atapendelewa kwenye mchakato huo.
Kutokana na malalamishi hayo, wadadisi wanasema kuwa mwelekeo huo unapaswa kumzindua mapema Dkt Ruto, kuwa kuna hatari ya chama hicho kupoteza umaarufu ikiwa hatadhibiti hali mapema.
“Ni wazi kuwa shughuli ya mchujo ndio mtihani mkubwa zaidi wa kisiasa unaomwandama Dkt Ruto. Ni suala ambalo litakijenga ama kukivuruga chama chake kabisa.,” asema Bw Felix Onyango, ambaye ni mdadisi wa siasa.
Katika kile kinachoonekana kuwa suala analolichukulia kwa uzito, Dkt Ruto alisema majuzi kwamba ndiye atayakechukua lawama zote ikiwa kutatokea matatizo katika mchujo wa chama.
“Nimekuwa nikiendesha shughuli za michujo ya vyama kwa karibu miaka 25 iliyopita. Hivyo, nina ujuzi wa kutosha. Ili kuepuka matatizo yaliyoshuhudiwa awali, nitachukua udhibiti wa zoezi hilo kwa kutumia tajriba niliyo nayo,” akasema kwenye mahojiano.
Hata hivyo, baadhi ya wawaniaji wanaotafuta tiketi za chama wanadai “wapo maafisa wenye ushawishi ambao washaamua watu watakaopewa tiketi.”
“Kuna watu tunaojua ambao tayari washapata tiketi. Inasikitisha kuwa Dkt Ruto bado hana ufahamu kuhusu uhalisia wa jinsi hali ilivyo katika maeneo ya mashinani,” akasema mwaniaji ambaye hakutaka kutajwa.
Wadasisi wanasema kwamba ikizingatiwa lengo la Dkt Ruto ni kuijenga UDA kuwa chama cha kitaifa, lazima ahakikishe “laana” iliyoikumba Jubilee kwenye teuzi za 2017 haimfuati tena.
Wanasema kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee itakayomhakikishia kuwa UDA itapanuka na kufikia hadhi ya ilivyokuwa Kanu wakati wa enzi za Mzee Jomo Kenyatta au marehemu Daniel Moi.
“Dkt Ruto ana lengo zuri sana, kwani vyama vingi nchini ni vya kimaeneo na kikabila. Hata hivyo, usimamizi wa shughuli za uteuzi ndio utakaoamua ikiwa ndoto yake itatimia au la,” asema Bw Kiprotich Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.