Wanaume watalimana leo Stamford Bridge
NA MASHIRIKA
CHELSEA watakuwa wenyeji wa Liverpool katika gozi kali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), ugani Stamford Bridge hii leo Jumapili.
Everton nao wataalika Brighton uwanjani Goodison Park, Brentford wapepetane na Aston Villa huku Burnley ikiwaendea Leeds United ugani Elland Road.
Mechi iliyokuwa ikutanishe Newcastle United na Southampton uwanjani St Mary’s imeahirishwa, kutokana na ongezeko la visa vya majeraha na maambukizi ya virusi ya corona kambini mwa Newcastle.
Pambano hilo lilikuwa la 17 kuahirishwa katika EPL tangu Desemba.
Sawa na Liverpool waliopokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Leicester katika mchuano uliopita ligini; Chelsea nao watakuwa na kiu ya kujinyanyua baada ya Brighton kuwalazimishia sare ya 1-1 katika mechi ya awali.
Kujikwaa zaidi kwa Chelsea au Liverpool kutadidimiza matumaini yao ya kufukuzia vinara Manchester City, wanaopigiwa upatu wa kuhifadhi ufalme wa EPL muhula huu chini ya mkufunzi Pep Guardiola.
Mechi nne kati ya tano zilizopita ambazo Chelsea wametandaza katika EPL ugani Stamford Bridge zimekamilika kwa sare za 1-1, huku The Blues wakikosa kukamilisha mchuano wowote bila ya kufungwa.
Japo kocha Thomas Tuchel amepuuza uwezekano wa Chelsea kutawazwa wafalme wa EPL msimu huu, baada ya uthabiti wa kikosi chake kulemazwa na majeraha pamoja na virusi vya corona, mkufunzi Jurgen Klopp amewataka masogora wake wa Liverpool kujituma maradufu.
“Kampeni za EPL zimefikia katikati na chochote kinaweza kutokea,” akasema Klopp.
Kichapo ugani King Power kilikuwa cha pili kwa Liverpool kupokea katika mashindano yote ya msimu huu wa 2021-22.
Mabingwa hao wa 2019-20 sasa wanakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 41, moja pekee nyuma ya Chelsea walioshinda EPL mara ya mwisho mnamo 2016-17 chini ya kocha Antonio Conte wa Tottenham Hotspur.
Kinachotarajiwa kuwapa Chelsea motisha zaidi ni rekodi duni ya Liverpool jijini London.
Kufikia sasa, mabingwa hao mara 19 wa EPL wameshindwa kuangusha Brentford, West Ham United na Tottenham Hotspur wanaotokea London katika mechi za ugenini muhula huu.
Hata hivyo, Liverpool wamepoteza mechi mbili pekee kati ya 11 zilizopita dhidi ya Chelsea ugani Stamford Bridge.
RATIBA YA EPL (Leo Jumapili)
Brentford vs Aston Villa (5:00pm) Everton vs Brighton (5:00pm)Leeds vs Burnley (5:00pm) Chelsea vs Liverpool (7:30pm
Jumatatu
Man-United vs Wolves (8:30pm)