Connect with us

General News

Wanaopinga Achani kuwania ugavana Kwale wakejeliwa – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wanaopinga Achani kuwania ugavana Kwale wakejeliwa – Taifa Leo

Wanaopinga Achani kuwania ugavana Kwale wakejeliwa

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Kwale Salim Mvurya amewapuuza wanaopinga azma ya naibu wake Fatuma Achani kumrithi ya kwa misingi ya jinsia, kabila na chama cha kisiasa.

Gavana Mvurya amewaambia wakazi kuwa kiongozi bora ni yule anayehubiri uwiano, umoja na maendeleo wala si kugawanya watu kisiasa.

Badala yake amewataka wakazi kumpigia kura naibu wake ambaye analenga kumrithi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Amewataka wapigakura kuchagua viongozi kulingana na maadili mema na maendeleo badala ya kabila, chama cha kisiasa na jinsia.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Makatibu Wakuu Prof Hamadi Boga na mwenzake wa Masuala ya Gerezani Bi Safina Kwekwe kutangaza hadharani kwamba watagombea ugavana.

Bi Kwekwe atakuwa naibu wa Prof Boga.Wagombea wengine ni pamoja na waziri wa zamani Chirau Mwakwere (Wiper), mfanyabiashara Daniel Dena (KANU), Spika wa Bunge la Kaunti ya Kwale Sammy Ruwa (ODM) na Bw Lung’anzi Mangale.

Lakini Bw Mvurya ambaye anapigia debe uongozi wa wanawake anataka wakazi wa Kwale kumchagua naibu wake ambaye ni kati ya wanawake watano wanaowania ugavana katika kaunti za Pwani.

Wengine ni mbunge wa Malindi Aisha Jumwa (Kilifi) kupitia UDA, Patience Nyange (Taita Taveta) kupitia Wiper, Umra Omar (Lamu), Ruweida Obbo (Lamu), Rachel Mwakazi (Taita Taveta).

“Kwale imepata maendeleo kwa sababu ya uongozi wetu bora na naibu wangu ataendeleza ruwaza yetu ya kufanikisha Kwale,” alisema Mvurya ambaye Bi Achani amekuwa naibu wake tangu mwaka wa 2013.

Naye Bi Achani amewashtumu viongozi wanaopinga uongozi wa wanawake kwa misingi ya kidini. Amewataka wakazi kuona mfano wa Tanzania ambapo Rais Samia Suluhu Hassan ni mwanamke Mwislamu.

Bi Achani ambaye aliidhinishwa na Naibu wa Rais William Ruto kugombea kiti hicho kwa tiketi ya UDA alisema wanawake hawawezi kugombea nyadhifa za uongozi kwenye misikiti.

“Lakini kwenye uongozi mwingine kando na msikitini hakuna tatizo. Kuna wanawake wengine ambao wanawania viti vya kisiasa, mbona mnilenge mimi kwa misingi ya dini? Si Rais Samia ni Muislamu?” aliuliza.

Kuingia kwa Prof Boga na Bi Kwekwe kwenye kinyanganyiro cha kumrithi Mvurya kumeleta taharuki katika siasa za Kwale hasa katika chama cha ODM.

Hata hivyo, baadhi ya wazee wa Kaya wameshawatawaza Prof Boga na Bi Kwekwe wakimsihi Bw Odinga awaunge mkono.

Bw Mvurya aliwasihi wakazi kujiandikisha kuwa wapigakura ili kuongezea nafasi ya Bi Achani ushindi.

“Serikali ya kaunti imeleta maendeleo mengi sana ni wakati wa wakazi kuwa mabalozi wetu. Tukitaka tuendeleze maendeleo basi hatuna budi kushirikiana na naibu wangu,” akashauri.