Connect with us

General News

Amerika yaadhibu nchi 3 za Afrika kwa kukiuka haki – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Amerika yaadhibu nchi 3 za Afrika kwa kukiuka haki – Taifa Leo

Amerika yaadhibu nchi 3 za Afrika kwa kukiuka haki

Na AFP

SERIKALI ya Amerika imeadhibu Ethiopia, Guinea na Mali kwa kuziondoa katika Mkataba wa Kibiashara na Mataifa ya Afrika (AGOA) kutokana na ukiukaji wa haki za kibinadamu unaoendelea katika nchi hizo.

Mkataba wa AGOA ulianzishwa mnamo 2000 na serikali ya Rais Mstaafu Bill Clinton kuwezesha Amerika na Afrika kufanya biashara kwa urahisi.

Amerika, katika taarifa yake ilisema kuwa ilikerwa na mapinduzi ya serikali yaliyofanyika mwaka jana katika mataifa ya Mali na Guinea na ukiukaji wa haki za kibinadamu unaoendelea nchini Ethiopia kufuatia mapigano baina ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa kundi la Tigray People’s Liberation Front (TPLF).

“Amerika imetiwa wasiwasi sana na mabadiliko ya serikali yanayokwenda kinyume na katiba katika nchi za Guinea na Mali na uvunjwaji mkubwa wa haki zinazotambuliwa kimataifa za binadamu unaochochewa na serikali ya Ethiopia na pande nyingine wakati mzozo ukiongezeka kaskazini mwa Ethiopia,’ ikasema Amerika.

Mataifa yaliyo chini ya mkataba wa AGOA yanasafirisha baadhi ya bidhaa nchini Amerika bila kulipia ushuru.

Viwanda vya nguo nchini Ethiopia vimekuwa vikinufaika pakubwa na mkataba wa AGOA kwani vimekuwa vikisafirisha mavazi kwa wingi nchini Amerika bila kulipia ushuru.

Punguzo hilo la kodi linaandamana na masharti kwamba serikali za mataifa husika zinaheshimu haki za binadamu, utawala bora na ulinzi wa wafanyakazi pamoja na kutoweka marufuku ya ushuru kwa bidhaa za Amerika zinazoingia kwenye maeneo yao.

Uchumi wa Ethiopia tayari umezorota kutokana na vita kaskazini mwa nchi hiyo, janga la virusi vya corona na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu.

Rais Joe Biden alitishia kuyaadhibu mataifa hayo matatu mnamo Novemba mwaka uliopita.Serikali jana ilisema agizo hilo la Rais Biden sasa limeanza kutekelezwa.

‘Kila nchi ina jukumu la wazi la kufuata njia ya kurejeshwa kwenye AGOA na serikali ya Amerika itashirikiana na serikali zao kufikia lengo hilo,’ ikasema Amerika.

Novemba, wizara ya biashara ya Ethiopia ilisema ilifadhaishwa sana na tangazo hilo la Amerika, ikisema hatua hiyo ‘itayarejesha nyuma mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana na kuwaathiri vibaya wanawake na watoto.’

Kufikia mwaka 2020, mataifa 38 yalikuwa tayari kwenye mkataba wa AGOA.Mkataba huo uliboreshwa mwaka 2015 na Seneti ambalo pia liliuongezea muda hadi mwaka 2025.

Hayo yanajiri huku uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwezi ujao kupisha utawala wa kiraia ukiwa hatarini kukosa kufanyika.

Kiongozi wa serikali ya mpito, Kanali Assimi Goita, sasa anataka aendelee kusalia mamlakani kwa miaka mitano.

Mali ilitoa pendekezo hilo kwa majirani zake wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS).Waziri wa Mambo ya Nje Abdoulaye Diop alitoa wito huo kupitia kituo kinachoendeshwa na serikali baada ya mkutano na rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo, ambaye pia ni mwenyekiti wa ECOWAS.

Awali, serikali ya mpito ilikubali kuandaa uchaguzi wa urais na ubunge Februari 2022, miezi 18 baada ya Kanali Goita kuongoza mapinduzi dhidi ya Rais Boubacar Ibrahim Keita.Tangu wakati huo kumekuwa na maendeleo kidogo katika maandalizi ya uchaguzi huku wakisema kunatokana na mivutano na ghasia kutoka kwa makundi ya wapiganaji wa Kiislamu.Guinea sasa inaongozwa na Kanali Mamady Doumbouya ambaye aliongoza mapinduzi dhidi ya Rais Alpha Conde, Septemba mwaka jana.Conde alibanduliwa mwaka mmoja baada ya kushinda urais kwa muhula wa tatu wa miaka mitano baada ya kupata asilimia 59.5 ya kura.