Joho alilia Raila amteue kuwa mgombea mwenza debeni
Na WINNIE ATIENO
GAVANA wa Mombasa Ali Hassan Joho, amemtaka kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kumteua kuwa mgombea mwenza kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 mwaka huu.
Sawa na wagombeaji wengine wa urais, Bw Odinga anayegombea urais kwa mara ya tano, hajataja mgombea mwenza.
“Ninamwambia Bw Odinga, wakiendelea anaweza kunichagua mimi kuwa mgombea mwenza. Nina uwezo wa kuwa Naibu wa Rais. Kwa miaka 10, nimekuwa gavana lakini hivi karibuni nitakuwa raia wa kawaida,” alisema Bw Joho.
Akiongea kwenye sherehe za kuadhimisha Mwaka Mpya katika bustani ya Mama Ngina Waterfront, Bw Joho alichukua fursa hiyo kuwaaga wakazi wa Kaunti ya Mombasa.Bw Joho ambaye anahudumu muhula wa pili na wa mwisho kama gavana kulingana na katiba, alisema anapania uongozi wa juu.
Mnamo Septemba mwaka jana, Bw Joho alikubali kutowania tiketi ya urais kwa chama cha ODM, ili kumwachia Bw Odinga baada ya kinara huyo wa ODM kumuahidi nafasi ya juu zaidi serikalini.
Duru zinadai kuwa aliahidiwa wadhifa wa uwaziri katika serikali ya kitaifa Bw Odinga akishinda urais.Hata hivyo, gavana huyo alionekana kushikilia matumaini ya kuwania urais, akieleza kuwa atagombea kwenye uchaguzi mkuu mwaka wa 2027.
“Sitakuwa kwenye kinyang’anyiro mwaka huu, lakini ninampigia debe Bw Odinga. Lakini mwaka 2027, utakuwa mwaka wangu, nitagombea urais. Ingelikuwa si watu wangu wa Mombasa kunishika mkono nisingelikuwa hapa. Ninawashukuru sana na ninawapenda,” alisema Bw Joho.
Bw Joho alijitosa kwenye ulingo wa siasa mwaka wa 2007 kama mbunge wa Kisauni. Mwaka wa 2013 alichaguliwa gavana na amehudumu kwa mihula miwili akitarajiwa kuondoka mwaka huu kulingana na katiba.Kadhalika Bw Joho alizisihi jamii za Mombasa kuendelea kuishi kwa umoja na amani.
“Napenda Kaunti ya Mombasa sababu ya jamii zetu ambazo zinaishi kama ndugu, kwa umoja na utangamano. Kuna kabila zote lakini tunaishi kama ndugu,” alisema.
Mwezi uliopita, Bw Joho alimtaja Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, kuwa mrithi wake.Awali Bw Joho alikuwa amesema hangemwidhinisha kiongozi yeyote akiwataka naibu wake Dkt William Kingi, Bw Nassir na mfanyibiashara Suleiman Shahbal, kupambana kwenye ulingo wa kisiasa.
Hata hivyo, mnamo Disemba 18, alibadilisha nia na kumpiga jeki Bw Nassir katika azma yake ya kuwania ugavana wa Mombasa.
Akiongea kwenye maadhimisho ya kuwasha taa ya mti wa Gavana wa Krisimasi katika eneo la Treasury Square, Bw Joho alisema tayari ashatoa mwongozo kuhusu mrithi wake.
Wagombea wengine wa ugavana ni pamoja na mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, aliyekuwa mbunge wa Nyali, Bw Awiti Bolo , Bw Mohammed Bahaidar na Dkt Sanjeev Agwaral ambao tayari wameanza kampeni kabambe mashinani.
Next article
Baraza la Wazee kukagua wagombea viti kabla ya uchaguzi