TAHARIRI: Benki ziboreshe mitambo yake kuokoa wateja
NA KITENGO CHA UHARIRI
WAKATI huu ambapo wazazi wengi wanawarudisha wanao shuleni, kuna haja kwa benki nchini kubuni mikakati ya kuhakikisha kuwa pesa ambazo wazazi wanaweka au kutoa kwenye akaunti zao ziko salama.
Hili ni baada ya kuibuka wahalifu waliobuni njia ambapo wanashirikiana na baadhi ya wafanyakazi wa benki husika kuingilia akaunti za wateja wao na kutoa pesa walizoweka.
Kwenye njama hiyo, wahalifu hao hutumia ujuzi wa kiteknolojia kuingia katika akaunti hizo ambapo huondoa pesa za wateja bila kuingiliwa kwa namna yoyote ile.
Imebainika pia wahalifu wanaweza kuingia kwenye akaunti hizo kwa kutumia kadi za ATM za wateja zilizopotea bila ufahamu wao.
Ijapokuwa uhalifu huu umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu, wataalamu wanaonya kuwa kiwango chake kimeongezeka katika siku za hivi karibuni kutokana na ukuaji wa teknolojia nchini na duniani kote.
Wanasema wadukuzi hao wanaweza kupata maelezo ya kifedha kuhusu mteja kwa kutumia Sh100 pekee.
Ni baada ya hapo ambapo hutumia maelezo hayo kuvuruga hali za kifedha za wateja hao.Katika hali hii, ni dhahiri kuwa lazima benki zote nchini ziimarishe usalama wa mitambo yake dhidi ya kuingiliwa na wahalifu hao.
Wazazi wengi huamini benki kama taasisi salama za kifedha ambako wanaweza kulipia karo za wanao bila matatizo yoyote.
Kutokana na ukuaji wa teknolojia, shule nyingi zimebuni mfumo ambapo mwanafunzi hutakikana tu kuwasilisha risiti kuonyesha kuwa amelipa karo ili kuruhusiwa kurejelea masomo.
Mbali na wazazi, wafanyabiashara wengi hutumia benki kuwekea fedha, ili kuwasaidia kuendesha shughuli muhimu zinazohusu biashara zao.
Haya yote yanapaswa kuwazindua wasimamizi wote wakuu wa benki kuwa wahalifu wengi hutumia wakati huu kujitajirisha, kwani wanafahamu baadhi ya wazazi huwa hawana ufahamu wowote kuhusu masuala ya kifedha.
Lazima pia wahakikishe wafanyakazi wao ni waadilifu, kwani si mara moja baadhi yao wamenaswa wakiwasaidia wahalifu kutekeleza visa vya wizi katika benki na kufanikiwa kuiba mamilioni ya pesa.
Je, litakuwa pigo la kiwango kipi ikiwa wahalifu hao watafanikiwa kuingia kwenye akaunti ambapo taasisi muhimu kama shule zinawekea fedha zao?
Mojawapo ya matokeo ni kufungwa kwa taasisi hizo, kwani hazitakuwa na fedha zozote za kuendeshea shughuli zake. Katika matukio kama hayo, watakaoathiriwa moja kwa moja ni wanafunzi, kwani watatatizika kimasomo.
Jasho la wazazi kuwatafutia wanao karo nalo litakuwa limepotelea chini.Ili kuepuka matukio kama hayo, benki hazina lingine ila kuhakikisha ni watu husika pekee wanaoweza kuingia kwenye mitambo hiyo.
Next article
ANC yasema haitishwi na Savula kujiunga na Azimio la Umoja