Connect with us

General News

Mianya ya pembejeo bandia yazibwa kampuni zikikumbatia mifumo ya kidijitali – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mianya ya pembejeo bandia yazibwa kampuni zikikumbatia mifumo ya kidijitali – Taifa Leo

Mianya ya pembejeo bandia yazibwa kampuni zikikumbatia mifumo ya kidijitali

Na SAMMY WAWERU

HAFLA ya mwaka huu ya muungano wa watengenezaji na wafanyabiashara wa mbegu nchini (STAK) ilikuwa ya kipekee, kampuni za pembejeo zikitumia jukwaa hilo kuonyesha bidhaa zao.

Ikiwa ilifanyika katika makao makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro), Loresho, kiungani mwa jiji la Nairobi, ilileta pamoja kampuni za pembejeo na wakulima.

Baadhi ya wakulima wakisafiri kutoka maeneo kama vile Kilifi, Kakamega, Machakos, na Nakuru, walijumuika na kampuni hizo ambapo kando na kuuziwa pembejeo kwa bei nafuu, walipata mafunzo kitaalamu na keuelezea changamoto zao.

Mwenyekiti wa STAK, Kassim Owino akizungumza wakati wa maonyesho ya muungano huo, makao makuu ya Kalro, Loresho, Nairobi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Kuwepo kwa mbegu bandia na ambazo hazijaafikia ubora wa bidhaa, ni kati ya mahangaiko waliyoibua kuzingira soko zima la pembejeo wakilalamikia “huathiri uotaji wa mbegu, ukuaji na kiwango cha uzalishaji”.

“Mwaka wa 2019, nilikuza mahindi kwenye ekari moja na kuvuna magunia 15 pekee badala ya kati ya 25 – 30 mazao ya kawaida,” akasema Peter Ng’ang’a, mkulima kutoka Nakuru, akalalamikia upungufu huo kuchangiwa na mbegu feki.

Akikumbuka hasara aliyokadiria, mkulima huyo wa mahindi na mifugo anasema hakuwa amefanya uchunguzi wa duka la bidhaa za mimea na mifugo lililomuuzia mbegu.

Dkt Oscar Magenya, Karani Mtafiti wa Masuala ya Kilimo katika Wizara ya Kilimo akizungumza wakati wa maonyesho ya STAK, makao makuu ya Kalro, Loresho, Nairobi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Anasema, aligundua baadaye halikuwa limeidhinishwa na taasisi husika.

“Nilipoteza mahindi yenye thamani ya Sh75, 000,” akafichua.

Kuling’ana na Ng’ang’a, Kenya ilipothibitha kuwa mwenyeji wa ugonjwa wa Covid-19 Machi 2020, wahuni wa biashara ya pembejeo bandia “walipata jukwaa maalumu kuendeleza utapeli”.

Matatizo yake si tofauti na ya Florence Wayua, mkulima Machakos.

Kutoka kushoto, Mwenyekiti wa STAK, Kassim Owino, Naibu Mkurugenzi Mkuu Kalro – Kitengo cha mbegu, Dkt Philip Leley, Dkt Oscar Magenya, Karani Mtafiti wa Masuala ya Kilimo katika Wizara ya Kilimo na Duncan Ochieng’, Afisa Mkuu STAK, wakionyesha pakio la mbegu lenye stika ya Kephis, wakati wa maonyesho ya pembejeo katika makao makuu ya Kalro, Loresho, Nairobi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Florence hulima mahindi, mboga, na matunda kama vile ndizi na avocado, na pia nduma eneo la Mumbuni, na aliiambia Taifa Leo Dijitali wakati wa maonyesho hayo ya STAK, Makala ya 19, kwamba amepitia changamoto za kero ya mbegu bandia kwa zaidi ya miaka miwili.

“Mbegu feki zimeathiri kila mmea,” akateta.

Pandashuka hizo pia zimehangaisha kampuni zinazozalisha na kuuza mbegu, majina yazo yakipakwa tope.

“Tumeshuhudia visa vingi vya mbegu zetu kughushiwa, kiasi cha wateja kushindwa kutambua zile halali,” akaelezea Antonina Kandie, mtaalamu kutoka Kenya Seeds – Simlaw Seeds, eneo la Nairobi.

Antonina Kandie, mtaalamu kutoka Kenya Seeds – Simlaw Seeds, akionyesha kipakio cha mbegu za mahindi chenye stika ya Kephis, wakati wa maonyesho ya STAK, makao makuu ya Kalro, Loresho, Nairobi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Hata hivyo, changamoto zinazozingira wakulima na kampuni za pembejeo zinaelekea kufika ukingoni kufuatia kamepni inayoendelea kuondoa wahuni sokoni.

Kwa ushirikiano na wadau husika, STAK imeweka mikakati kabambe kuhakikisha wakulima wanaweza kuthibitisha uhalisia wa mbegu wanazonunua.

Oktoba 2016, muungano huo wenye washirika kutoka sekta ya umma na kibinafsi, ulizindua mtandao wa kidigitali na ambao wakulima wanahimizwa kuukumbatia wanaponunua mbegu.

Wawakilishi wa kampuni za pembejeo nchini wakionyesha vipakio vya mbegu vyenye stika ya Kephis, wakati wa maonyesho ya STAK, makao makuu ya Kalro, Loresho, Nairobi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Agro-tech, ni uvumbuzi ambao kwenye pakio la mbegu kuna stika ya Taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis), unaponunua mbegu ukihitajika kuikwaruza na kutuma kodi ya tarakimu 14 zinazojitokeza kwa nambari 1393 kuthibitisha uhalisia.

Teknolojia hiyo haitozi malipo wala ada kutuma ujumbe.

“Ikiwa maelezo kuhusu uundaji wa mbegu ulizonunua hayataonekana, tuma tarakimu hizo kwa Kephisi kupitia nambari 0705001393, hatua za kinidhamu na sheria zichukuliwe mara moja,” akasema Duncan Ochieng’, Afisa Mkuu STAK, akihimiza wakulima kukumbatia mfumo huo wa kidijitali.

Huku akitaja Kiambu, Narok na Uasin-Gishu kama kaunti gaidi katika kughushi mbegu, Ochieng’ alisema kufikia sasa jumla ya visa viwili vimeandikishwa.

Emmah Mwenda, mtaalamu kutoka Seed-Co Kenya, akionyesha kipakio cha mbegu za mahindi chenye stika ya Kephis, wakati wa maonyesho ya STAK, makao makuu ya Kalro, Loresho, Nairobi. PICHA/ SAMMY WAWERU

“Stika za Kephis zimesaidia visa vya utapeli kupungua,” akasema Antonina Kandie, mtaalamu kutoka Simlaw Seeds na ambaye husimamia Kaunti ya Nairobi, Kiambu na Kajiado.

Afisa huyo alisema kampuni hiyo pia hutumia nambari za usajili za vipakio vyake vyake vya mbegu kuzifuatilia.

“Mkulima anapolalamikia kuhusu mbegu, huwa tunafanya uchunguzi kupitia nambari za vipakio,” akaongeza Daniel Mugo, mtaalamu wa mauzo kutoka East Africa Seeds, eneo la Mlima Kenya.

Mkulima (kushoto) akiwa na mtaalamu kutoka East Africa Seeds, wakionyesha vipakio vya mbegu za mahindi vyenye stika ya Kephis, wakati wa maonyesho ya STAK, makao makuu ya Kalro, Loresho, Nairobi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Kauli yake ilipigwa jeki na Samson Ndung’u, kutoka Seed-Co Kenya.

“Kupitia stika za Kephis, tumeweza kuhudumia wateja wetu ipasavyo. Tunaomba teknolojia ya lebo iboreshwe zaidi,” Ndung’u akasema.

Akipongeza teknolojia hiyo, Veronica Kimethu, mkulima kutoka Nakuru alisema ameweza na kufanikiwa kukwepa kero ya utapeli wa mbegu bandia.

“Hii ni hatua mahususi katika sekta ya kilimo. Wahuni wasipewe mwanya, wakulima wamehangaika vya kutosha kwa muda mrefu kupitia mbegu feki,” akasema mkulima huyo wa mahindi na mifugo.

Mtaalamu Emmah Mwenda, kutoka Seed-Co Kenya, akionyesha mazao yaliyozalishwa kupitia mbegu zilizoidhinishwa na Kephis, wakati wa maonyesho ya STAK, makao makuu ya Kalro, Loresho, Nairobi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Wakati wa maonyesho hayo yenye mada: “Technological Innovation and Increased Seed Production for Food Security and Improved Livelihoods”, mwenyekiti wa STAK, Kassim Owino alidokeza kwamba washikadau husika wanashirikisha idara ya mahakama wanaounda na kuuza mbegu feki kuchukuliwa hatua kali kisheria.

“Faini inayotozwa wanaopatikana na hatia, ni sawa na tone la maji baharini. Wanapaswa kupashwa adhabu ambayo itatuma ujumbe wa onyo kwa wahusika wahuni wenza,” Owino akaelezea, akiahidi jitihada za STAK kuhakikisha kuwepo kwa mbegu halisi nchini na zilizoafikia ubora wa bidhaa.

Alisema muungano huo unashirikiana kwa karibu na Kalro, na wazalishaji wa mbegu nchini, kupata bidhaa bora kupitia mifumo ya teknolojia za kisasa na Kisayansi.

Wakulima, Peter Ng’ang’a (kushoto) na Veronica Kimethu, wote kutoka Nakuru wakionyesha vipakio vya mbegu vyenye stika ya Kephis, wakati wa maonyesho ya STAK, makao makuu ya Kalro, Loresho, Nairobi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Kuna jumla ya kampuni 153 zinazotengeneza mbegu nchini, na afisa huyo alisema sheria imeweka wazi lazima zitumie stika za Kephis.

Dkt Oscar Magenya, Karani Mtafiti wa Masuala ya Kilimo katika Wizara ya Kilimo aidha alisema serikali imeweka mikakati bulibuli kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na zilizoidhinishwa.

“Serikali inafanya kila iwezalo kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zilizoafikia ubora wa bidhaa na kuidhinishwa na asasi husika, ili kuimarisha sekta ya kilimo nchini,” Dkt Magenya akasisitiza.

Alidokeza kwamba kwa sasa, inatathmini kupunguza au hata kuondoa ushuru (VAT) unaotozwa mbegu za mboga.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending