Connect with us

General News

Huu mwasho kwenye nyeti zangu ni kitu gani? – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Huu mwasho kwenye nyeti zangu ni kitu gani? – Taifa Leo

DKT FLO: Huu mwasho kwenye nyeti zangu ni kitu gani?

Mpendwa Daktari,

Mimi ni mwanamke anayekaribia miaka 40. Nimekuwa nikikumbwa na mwasho katika sehemu inayozingira uke wangu. Pia nimekuwa nikitokwa na majimaji mazito ukeni mfano wa ute wa yai. Tatizo laweza kuwa nini?Virginia, Mombasa

 

Mpendwa Virginia,

Ni kawaida kwa wanawake wote baada ya kutimu umri wa kubalehe kutokwa na majimaji ukeni. Kwa kawaida huu huwa mchanganyiko wa majimaji na seli ambazo husaidia kudumisha usafi na unyevu ukeni, na hivyo kuzuia maambukizi.

Mara nyingi sura ya majimaji hayo hubadilika kuambatana na mzunguko wa hedhi, mazoezi, matumizi ya dawa za kihomoni, vile vile msisimko wa tendo la ndoa. Majimaji hayo yaweza kuwa meupe, maang’avu, mazito au mepesi kuambatana na wakati tofauti wa mzunguko wa hedhi.

Pia, ni kawaida kushuhudia majimaji ya rangi ya kahawia, kabla, wakati wa na baada ya hedhi, na hata wakati mwingine katikati ya kipindi cha hedhi.

Ikiwa majimaji hayo sio ya rangi ya kawaida (manjano, kijani na wakati mwingine meupe), kuna mwasho, harufu mbaya au majimaji mazito, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba umekumbwa na maambukizi ya ukeni.

Maambukizi haya yaweza kuwa kutokana na ukuvu (kama vile candidiasis), bakteria au viumbehai vingine. Kwa upande wako, kuna uwezekano mkubwa kwamba una candidiasis.Litakuwa jambo la busara kukaguliwa na daktari na pia kufanyia uchunguzi wa majimaji hayo.

Ikiwa itathibitishwa kwamba una candidiasis, basi utapewa dawa za kukabiliana na ukuvu. Maambukizi mengine yoyote pia yatatibiwa vilivyo.

Maambukizi yoyote yaweza sambazwa, japo sio kawaida kusambaza candidiasis kutoka kwa mwanamke hadi kwa mwanamume, na ikiwa mwenzio aliambukizwa na hakutibiwa basi atakuambukiza tena.

Zingatia usafi na unapojipangusa, fanya hivyo kuanzia mbele ukielekea nyuma, usitumie vyoo vichafu, valia suruali za ndani za kitambaa cha pamba, usivalie suruali zinazobana, na ikiwezekana kuwa na mazoea ya kulala bila nguo za ndani.

Pia, tumia viuavijasumu ikihitajika. Iwapo unakumbwa na candidiasis kila unapotumia viuavijasumu, litakuwa jambo la busara kutumia dawa za kukabiliana na ukuvu, kila unapokamilisha dozi ya viuavijasumu.