Connect with us

General News

Biashara ikinoga, kwa siku anaingiza Sh50,000 – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Biashara ikinoga, kwa siku anaingiza Sh50,000 – Taifa Leo

Biashara ikinoga, kwa siku anaingiza Sh50,000

NA MWANDISHI WETU

KIPINDI akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi miaka ya 90, Joel Njue alipenda sana somo la kutengeneza vitu mbali mbali kwa kutumia mikono yake.

Na wala hakuwa na habari kwamba somo hilo lingemfaa pindi amalizapo masomo yake ya upili na kuanza mishemishe zake za kujisakia mkate wake wa kila siku.

Mara baada ya kukamilisha masomo yake ya upili katika shule ya Meru Boys mwaka wa 2003, Njue,34 aliamua kufululiza moja kwa moja hadi Mombasa kusaka ajira.

“Sikujaliwa kujiunga na chuo chochote kuendeleza masomo yangu baada ya kukamilisha kidato cha nne kutokana na hali ngumu ya kimaisha, “ asema Njue wakati wa mahojiano na AkiliMali.

Aidha baada ya kutua Mombasa, Njue alijifunza kuendesha pikipiki na baada ya kipindi kifupi tu akajitosa katika biashara ya uchukuzi kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda.

Ni kazi aliyoifanya kwa bidii huku akiweka akiba na kujitengea muda wa kufanya mazoezi ya kujenga misuli akilenga kuajiriwa kama baunsa katika hoteli za kitalii, Pwani.

Mwaka wa 2011, alifanikiwa kuajiriwa kama baunsa katika klabu ya Bob’s iliyoko eneo la Nyali, mojawapo ya klabu maarufu Mombasa kipindi hicho.

Ni kazi aliyofanya kwa kujituma na mwaka wa 2015 wasimamizi wa klabu ya Yulls iliyo ufuoni eneo la Shanzu walivutiwa na uadilifu wake kazini na kuamua kumuajiri kama mojawapo ya baunsa wa klabu hiyo.

“Nilikuwa nikifanya ubaunsa usiku na wakati wa mchana ninapata muda wa kutengeneza viti, meza kwa kutumia miti na wakati mwingine kuunda vikapu kwa kutumia miyaa,” asimulia Njue.

Kila baada ya kumaliza kuunda vifaa hivi nilikuwa na mazoea ya kuvipiga picha kisha usiku nikiwa katika kazi yangu ya ubaunsa ninawaonesha wateja watalii kazi zangu na wengi walizichangamkia kwa kuzinunua.

Ni biashara iliyompatia mapato ya ziada mbali na kazi yake ya ubaunsa iliyomletea hela si haba.Hata hivyo, mambo yalimwendea kombo, mapema mwaka jana wakati wa mlipuko wa virusi vya corona ambapo alijipata akipoteza kazi yake kama baunsa baada ya kuhudumu kwa kipindi kirefu.

Baada ya kupoteza kazi, Njue hakukata tamaa bali aliamua kuvalia njuga kazi yake ya kuunda viti, meza, vikapu, teo miongoni mwa vifaa mbali mbali kwa kutumia miti na miyaa.

“Niliamua kutumia akiba yangu ya Sh20,000 kama mtaji ya kuanzishia biashara yangu kwa kununua malighafi,” asimulia Njue anayeendesa biashara yake kandokando mwa barabara ya Mombasa-Malindi, mkabala na mzunguko wa barabara ya kuelekea mtambo wa kutengeza simiti ya Bamburi, Mombasa.

Kwa mujibu wa Njue, ili kuunda kiti, meza ama kifaa cha kuangikia vyatu ama nguo iliyo madhubuti, anachoma kwanza miti yake aina ya muarubaine katika moto wa kadri kisha anaiondoa na kuinyorosha kabla ya kuanza kuunda kifaa anachodhamiria kuunda.

Kwa kifaa cha kuangikia nguo ama viatu, humchukua takribani muda wa saa mbili pekee kuwa tayari kisha anaking’arisha vyema kwa rangi aipendayo mteja wake.

Kuna pia vikapu vikubwa na vidogo, mikeka, kofia ambavyo ameongeza katika biashara yake na vinavyovutia wateja kibao.

Njue hata hivyo anafichulia Akimali kwamba aghalabu hununua aina ya mikeka maalum kutoka Meru na kuwauzia wateja wake.

Kifaa cha ya kuangikia nguo anauza kwa kati ya Sh3,500 hadi Sh4,500 wakati cha viatu ni kati ya Sh2,000 hadi Sh2,500.Mkeka anauza kwa Sh600 huku kikapu akiuza kulingana na ukubwa kuanzia Sh250 hadi Sh400 , teo Sh300 na teo zenye mapambo huziuza Sh450.

Kulingana naye, biashara ikinoga hakosi kitita cha Sh50,000 kwa siku wakati biashara ikiwa mbaya anarudi nyumbani na Sh18,000.

Njue anakiri kazi yake ya awali ya ubaunsa ya mwezi inalipwa na biashara yake ya siku tatu pekee akiapa kutorudia kazi hiyo hata kama hali itarudi shwari.

Asema mwanzoni baadhi ya vijana aliokuwa akifanya nao kazi ya ubaunsa walimbeza walipomwona akifanya kazi hiyo ila kwa sasa wanajuta baada ya kuwachishwa kazi ghafla baada ya mlipuko wa corona.

Katika kipindi kifupi alichojitosa mzimamzima katika biashara hii, ameweza kujiwekea akiba nzuri mbali na kuwasaidia nduguze wadogo kupata masomo yao ya upili.

Anawaasa vijana kuwa wabunifu kwa kujifunza kazi za kujitegemea na wala siyo kutegemea kazi za kuajiriwa zinazoweza kuisha ghafla.