Hofu yazuka kuhusu unga kupanda bei
Na WANDERI KAMAU
WASAGAJI mahindi nchini wameiandikia barua Wizara ya Kilimo, wakionya kuhusu ongezeko la bei ya unga kutokana na upungufu wa kiwango cha mahindi nchini.
Hilo ndilo linatajwa kuchangia ongezeko la bei ya gunia moja la mahindi la kilo 90.Kwenye barua kwa wizara hiyo, Muungano wa Wasagaji Mahindi Kenya (UGMA) ulisema kuwa kwa sasa, wasagaji wananunua gunia moja la mahindi kwa Sh3,000 ikilinganishwa na Sh2,800 hapo awali.
Muungano huo, ambao husambaza asilimia 80 ya unga wa mahindi nchini, unaitaka wizara kuchukua hatua za mapema kudhibiti bei hizo ili kuhakikisha haziongezeki.
Unasema serikali inapaswa kuwaokoa Wakenya kutokana na zigo la bei za juu za vyakula.“Tunaitaka serikali kujua kwamba bei ya unga itapanda kwa haraka katika siku chache zijazo kwani huenda bei ya gunia moja la mahindi ikafikia Sh3,500,” akasema Bw Ken Nyaga, ambaye ndiye mwenyekiti wa muungano huo.
Kinaya ni kuwa, uhaba huo unatokea huku msimu wa uvunaji mahindi ukiendelea katika kaunti za Uasin Gishu na Trans Nzoia, ambazo ndizo huzalisha zao hilo kwa wingi zaidi nchini.
Bw Tim Njagi, ambaye ni mtafiti wa kilimo katika Taasisi ya Utafiti na Sera ya Tegemeo iliyo eneo la Egerton, Nakuru, anasema kuna uwezekano uhaba huo umeletwa kimakusudi na baadhi ya wadau katika sekta ya usagaji.
Vile vile, anasema wakulima wengi hawataki kuyauza mahindi yao wakati huu kwani bei za zao hilo bado ziko chini.
“Kwa wakulima wengi, huo ni mkakati wa kibiashara. Wanataka kuyauza mazao yao wakati bei zitakapopanda ili kupata faida,” akasema.
Serikali hata hivyo imetabiri kuwa uzalishaji mahindi utapungua kwa asilimia 20 msimu huu, kutokana na mvua chache na athari za viwavijeshi walioyashambulia mashamba mengi ya zao hilo mwezi Machi.Tangu Januari, bei ya wastani ya pakiti ya kilo mbili ya unga imekuwa Sh100 kwenda juu.
Ikiwa serikali haitachukua hatua za mapema, ongezeko hilo linatarajiwa kuwaongezea Wakenya mzigo wa bei za juu za vyakula.
Next article
Michenza kitega uchumi tosha kwa mwalimu mstaafu