Kaunti 22 zilivyotafuna hela za wananchi
NA PETER MBURU
DALILI kuwa Wakenya wanaotarajia maendeleo kutoka kwa serikali za kaunti mwaka huu wa mwisho kabla ya uchaguzi wataambulia patupu zimejitokeza, baada ya kaunti kutumia takriban kila senti zinazopokea kujilipa mishahara, zikitelekeza miradi ya maendeleo.
Ripoti ya punde zaidi ya Mkaguzi wa Bajeti inaonyesha kuwa jumla ya kaunti 22 hazikutumia hata shilingi moja kufadhili maendeleo, licha ya kutia mifukoni mabilioni ambayo zilipokea na kushindwa kuokota ushuru kwa viwango vinavyofaa.
Ripoti hiyo iliyodadisi jinsi kaunti zilitumia pesa za bajeti miezi mitatu ya kwanza mwaka 2021/22 (Julai-Septemba 2021), inaonyesha kuwa kwa jumla, kaunti zilitumia asilimia 93 ya pesa kwa mishahara na marupurupu, huku miradi ya maendeleo ikitengewa chini ya asilimia sita pekee.
Kaunti ambazo hazikutenga hata shilingi moja ya pesa zilizopokea kufadhili maendeleo ni kama Baringo, Bungoma, Busia, Homa Bay, Isiolo, Kajiado, Kericho, Kilifi, Kisumu, Machakos, Marsabit, Migori, Mombasa, Nairobi, Nakuru, Narok, Nyandarua, Siaya, Taita-Taveta, Trans Nzoia, Vihiga na Wajir.
Kati ya Julai na Septemba, serikali za kaunti nchini zilipokea jumla ya Sh104.1 bilioni, kati ya Sh505.2 bilioni zinazotarajia kufikia Juni mwaka huu. Zilitumia Sh52 bilioni katika kipindi hicho, ripoti ya Mkaguzi wa Bajeti inaonyesha.
“Jumla ya pesa zilizotumiwa na serikali za kaunti katika kipindi cha robo ya kwanza mwaka 2021/22 ni Sh52.8 bilioni. Kaunti zilitumia Sh49 bilioni ama asilimia 93.3 ya matumizi yote kwa mishahara na marupurupu,” Mkaguzi wa Bajeti Margaret Nyakang’o akasema.
Pesa hizo ni ongezeko la Sh14 bilioni (ama asilimia 40), ikilinganishwa na Sh35.8 bilioni ambazo kaunti zilitumia kwa mishahara na marupurupu kipindi sawa na hicho mwaka 2020/21.
Kati ya Sh49 bilioni hizo, Sh38 bilioni zilitumika kwa mishahara, huku Sh11 bilioni zikitumika kwa marupurupu kama ya usafiri.
Kaunti zote 47 zilitumia Sh3.5 bilioni pekee kufadhili maendeleo, ama asilimia 1.9 ya pesa zinazofaa kutumika mwaka 2021/22.
Ni kaunti tatu pekee, Kitui, Kakamega na Kisii ambazo Bi Nyakang’o anaripoti kuwa zilitengea miradi ya maendeleo kiwango cha pesa cha kuridhisha, kwa kati ya asilimia 8 na 12 ya bajeti zao za mwaka.
Kaunti za Mandera, Siaya na Narok aidha zilitumia kati ya asilimia 20 na 28 ya matumizi yote kipindi hicho kufadhili maendeleo.
Ripoti hiyo vilevile inaonyesha kuwa licha ya kutumia kiwango kikubwa cha pesa kwa mishahara- kinyume na sheria kuhusu usimamizi wa pesa za umma- kaunti zilishindwa kukusanya ushuru kwa kiwango kinachofaa ili kuendesha majukumu yao.
Kaunti zote 47 zilikusanya jumla ya Sh6.76 bilioni kati ya Julai na Septemba, asilimia 12 ya kiwango kinachohitajika mwaka mzima wa 2021/22. Ili kukusanya kwa kiwango kinachohitajika na kulingana na malengo kwenye bajeti, kaunti zilifaa kukusanya angalau Sh14.1 bilioni kati ya Julai na Septemba.
“Udadisi wa ushuru wa kaunti unaonyesha kuwa kaunti zilizokusanya pesa chache zaidi zilikuwa Kisumu (asilimia 7), Nairobi (asilimia 7) na Murang’a (asilimia 6),” Bi Nyakang’o akasema.
Kaunti zilizojikakamua na kukusanya ushuru wa kuridhisha ni Migori, Turkana na Samburu, zikiokota kati ya asilimia 29 na 30 ya ushuru ambao zinalenga mwaka huu.
“Ili kurekebisha changamoto zilizoshuhudiwa, Mkaguzi wa Bajeti anashauri kaunti kuhakiki malengo ya ushuru zinaotarajia kukusanya kuwa yanayoweza kutekelezwa,” ripoti hiyo ikasema.
Mkaguzi wa bajeti aidha alifichua kuwa wawakilishi wodi (MCAs) kati ya Julai na Septemba walijilipa Sh57 milioni kwa marupurupu ya kushiriki vikao, zaidi ya kiwango walichopokea katika kipindi sawa mwaka 2020/21.
“Katika kipindi hicho, mabunge ya kaunti yalitumia Sh433 milioni kwa marupurupu ya wawakilishi wodi, kati ya Sh2.48 bilioni zilizotengwa mwaka mzima,” ripoti ikasema.Baadhi ya mabunge ya kaunti ambayo yalitumia kiwango kikubwa ni Bungoma (asilimia 52 ya bajeti ya mwaka mzima), Kisumu (asilimia 49 ya bajeti) na Machakos (asilimia 35 ya bajeti).