Bei ya juu ya unga yalemea Wakenya
BARNABAS BII na CECIL ODONGO
WAKENYA watalazimika kujifunga mshipi kupambana na makali ya njaa kufuatia kupanda kwa bei ya unga.
Hali hiyo ngumu imesababishwa na uhaba wa mahindi nchini.Bei ya pakiti ya unga wa kilo mbili ambayo miezi michache tu ilikuwa kati ya Sh90 na Sh108 maeneo mbalimbali nchini, sasa imepanda hadi kati ya Sh122 hadi Sh130 kwenye miji mingi.
Bei ya ‘gorogoro’ (mkebe wa kilo mbili) moja ya mahindi pia imepanda kutoka kati ya Sh80 na Sh100, mwezi uliopita, hadi Sh 130 na Sh150 katika maeneo mengi nchini.
Bei hiyo ya juu huenda ikawalemea Wakenya wengi wa mapato ya chini.Kupanda kwa bei ya unga kunajiri wakati ambapo Wakenya wakikabiliwa na hali ngumu ya kifedha baada ya kutumia hela nyingi katika sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.
Wazazi pia walitumia hela nyingi kulipia karo ya watoto wao hivyo kusalia pagumu.Msimu wa sherehe za Krismasi na mwaka mpya, Wakenya wengi huwa hawali ugali hasa wakipenda sana kula chapati inayotengenezwa kwa kutumia unga wa ngano pamoja na pia vitoweo vingi ambavyo huliwa kwa mchele.
“Mara nyingi Disemba watu hawali ugali ndio maana bei ilikuwa afadhali ila tunatarajia kuwa hitaji la unga wa kupikia ugali litaendelea kupanda ikizingatiwa msimu wa sherehe umetamatika. Katika siku chache zijazo tunataraji bei ya unga itapanda hata zaidi,” akasema Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Kampuni za Kusaga unga Ken Nyaga.
Kiini cha kupanda kwa bei ya unga ni uhaba wa mahindi hasa katika maeneo ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa na Magharibi ambayo huzalisha mahindi kwa wingi.
Kutokana na uhaba huo kumeibuka ushindani mkali kati ya Kampuni za kusaga mahindi na Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) katika ununuzi wa mahindi, baadhi ya wakulima nao wakihodhi mazao yao wakisubiri bei ipande hata zaidi.
“Bei ya unga inatarajiwa itaendelea kuwa juu kutokana na ukosefu wa mahindi ya kutosha sokoni. Hatuna budi ila kuongeza bei ya unga kwa sababu hata mahindi yanayowasilishwa kwetu hayatoshi na tunagharimika sana kuyanunua,” akasema mmiliki wa kampuni ya kusaga mahindi Eldoret, David Kosgey.
NCPB imekuwa ikinunua gunia la kilo 90 la mahindi kwa Sh3,000 ilhali hapo awali lilikuwa likinunuliwa kwa Sh2,700.
Wamiliki wa kampuni za kusaga unga nao wanatoza Sh3,200 na kuwavutia wakulima wengi zaidi kuliko NCPB.Wiki iliyopita, kampuni za kusaga mahindi ziliandikia Wizara ya Kilimo barua zikionya kuhusu uhaba wa mahindi waliodai unaendelea kuchangia kupanda kwa bei ya unga na kuwaumiza Wakenya.
Hata hivyo, kumeibuka madai katika Kaunti ya Trans Nzoia ambako kilimo cha mahindi huwa kimeshamiri kuwa hakuna uhaba wa mazao hayo, wakulima wakidaiwa kuwa na hazina ya kutosha.