Connect with us

General News

Wanyonge maskini wanavyopuuzwa – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wanyonge maskini wanavyopuuzwa – Taifa Leo

Wanyonge maskini wanavyopuuzwa

Masaibu ya wakazi wa mtaa wa mabanda wa Mukuru Kwa Njenga yanaonyesha jinsi maskini nchini wanavyochezwa na kukosa pa kukimbilia wakihangaishwa na kupuuzwa na serikali inayopaswa kuwalinda, wanaharakati wanasema.

Wanasema serikali inachofanya ni kuwacheza shere maskini inavyofanyia wanaohitaji msaada au kuhangaishwa na watu walio na ushawishi.

“Wanyonge hathaminiwi, hawana wa kuwajali na wanayopitia wakazi wa Mukuru Kwa Njenga, wazazi wa kijana aliyeachwa kwenye maporomoko ya mgodi eneo la Bondo, Siaya na wazazi wanaohangaishwa na walimu wakuu kwa kuongeza karo ni mifano tu ya kupuuzwa kwa wanyonge,” asema mwanaharakati Simon Mule.

Wakazi wa mtaa wa Mukuru Kwa Njenga wamekuwa wakiteseka baada ya nyumba walizokuwa wakiishi kwa zaidi ya miaka 50 kubomolewa na serikali kwa kile ilichodai kupisha ujenzi wa barabara.

Hata hivyo, ilibainika madai ya ujenzi wa barabara ilikuwa ni kisingizio tu, baada ya watu wenye ushawishi kuanza kupima ardhi hiyo kuigawa na wakazi wakazua ghasia zilizosababisha mtu mmoja kuuawa.

Wakazi hao wanasema walichezwa shere Alhamisi maafisa wa serikali walipowataka kujenga upya nyumba zao zilizobomolewa kisha wakatuma maafisa wa polisi usiku siku hiyo kuwapiga na kuwafurusha.

Hii ilikuwa saa chache baada Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiangi na mwenzake wa Ardhi Farida Karoney pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) Mohamed Badi kuwahakikishia hawatahamishwa.

“Tanauliza Kenya ina serikali ngapi? Waziri anatuhakikishia hatutahama na kisha polisi anaosimamia na maafisa wake wa utawala wanakuja usiku kutushurutisha tuhame. Nani atatuokoa?” alihoji Bw James Mbaka mkazi wa mtaa huo.

Bw Mbaka anasema wanayopitia wakazi wa mtaa wa Mukuru wa Njenga yanaonyesha kuna watu wenye nguvu wanaomezea mate ardhi hiyo.

“Sio ajabu hakuna mwanasiasa anayetetea wakazi hao. Ikiwa wanahangaishwa msimu wa uchaguzi mkuu na wanaogombea viti wamenyamaza, itakuwaje kipindi cha uchaguzi kikipita?” alihoji.

Katika kisa cha maporomoko ya mgodi wa dhahabu eneo la Abimbo, Bondo Kaunti ya Siaya, serikali imepuuza familia ya mvulana Tom Okwach ambaye mwili wake haujapatikana tangu Desemba 2 mwaka jana.

Familia hiyo imekuwa ikikesha kwenye eneo la mkasa huku serikali ikitoa visingizio vya kutosaidia kuopoa mwili wa mpendwa wao.

Hii ni tofauti na ilivyokuwa miaka miwili iliyopita jeshi lilipoopoa mwili wa mama na msichana gari lao lilipozama katika Bahari Hindi kwenye kivuko cha Likoni.

Wanaharakati wanasema kwamba serikali inayopaswa kuonyesha kwa vitendo imekuwa ikiendeleza zoezi la uhusiano mwema inapolaumiwa huku raia wanyonge wakiendelea kuhangaishwa na maafisa wa serikali, viongozi dhalimu na mabwanyenye wenye ushawishi.

Ingawa waziri wa elimu Profesa George Magoha ameonya walimu wakuu dhidi ya kuongeza karo, wazazi wanalalamika kuwa wanatakiwa kulipa ada zaidi.Katika baadhi ya shule, wazazi walilalamika kuwa wanatakiwa kulipa kati ya Sh3,000 na 9,000 zaidi ya karo iliyowekwa na serikali.

“Wanyonge kweli hawana wa kuwatetea. Tumelalamika kwa maafisa wa elimu lakini hakuna hatua zinazochukuliwa,” alisema mzazi mmoja mkazi wa Nairobi ambaye mtoto wake anasomea Embu na kuomba tusitaje jina lake mwanawe asidhulumiwe na wasimamizi wa shule.

Taswira nyingine ya mnyonge anavyochezwa inajitokeza katika maeneo yanayokubwa na usalama ambako maafisa wa serikali wanahimiza watu kurejea makwao au kupeleka watoto wao shuleni huku mashambulizi ya majangili yakiendelea licha ya serikali kudai imeimarisha usalama.

Hali hii inashuhudiwa katika maeneo ya kaunti za Pokot Magharibi, Turkana, Baringo, Samburu, Isiolo na Lamu. Katika baadhi ya maeneo, wakazi wanaishi kama wakimbizi wa ndani baada ya kutoroka makwao wakihofia usalama ambao serikali inafaa kuwahakikishia.