Hatua ya Washiali kujiondoa kuwania ubunge yauma UDA
Na CHARLES WASONGA
UAMUZI wa mwandani mkuu wa Naibu Rais William Ruto kutoka eneo la magharibi, Benjamin Washiali kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ubunge Mumias Mashariki imeibua hisia katika eneo hilo.
Hatua hiyo imeibua hofu ndani ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), tawi la Kakamega, huku baadhi ya wafuasi wakiitaja kama pigo kwa mustakabali wa chama hicho.
Kwanza, kuna wale wanaodai kuwa kujiondoa kwa Bw Washiali kutaaathiri nafasi ya chama hicho kupata idadi tosha ya viti vya ubunge kutoka kaunti ya Kakamega katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
“Sisi kama wafuasi wa UDA katika eneo bunge hili la Mumias Mashariki tumeingiwa na hofu kwani hatuna uhakika kwamba yule ambaye atateuliwa kupeperusha bendera ya chama chetu katika uchaguzi ataibuka mshindi. Tulikuwa na uhakika kwamba UDA ingepata kiti hiki kama Bw Washiali angewania kwani rekodi yake ya maendeleo ni nzuri,” akasema Bw Kennedy Lumbasi ambaye ni mshirikishi wa UDA, eneo bunge la Mumias Mashariki.
Duru zinasema kuwa mtaalamu wa masuala ya kifedha Peter Salasya ambaye Bw Washiali alimshinda katika uchaguzi mkuu wa 2017, amekuwa akiendesha kampeni kali kwa lengo la kumng’oa mbunge huyo.
Bw Salasya, ambaye aliwania kiti hicho kwa tiketi ya ODM, ameelezea imani kuwa atateuliwa tena na chama hicho mwaka huu.
Japo, Bw Washiali ametangaza wazi kwamba ataelekeza juhudi na nguvu zake katika kampeni za kumpigia debe Dkt Ruto, wadadisi wanasema angemfaidi Naibu Rais zaidi ikiwa angewania ubunge.
“Ni rahisi kwa mgombeaji ubunge kwa chama fulani kuwashawishi wafuasi wake kumpigia kura mgombeaji urais wa chama chake ikilinganishwa na mtu ambaye hayuko kinyang’anyiro,” anasema Bw Martin Andati.
“Kwa hivyo, bila shaka hatua ya Washiali kujiondoa uchaguzini itaathiri kampeni za Dkt Ruto katika eneo bunge hilo ikizingatiwa kuwa Bw Washiali ni mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa zaidi,” anaongeza mchanganuzi huyo wa masuala ya kisiasa.
Mnamo Jumatatu Bw Washiali aliwaambia wafuasi wake kwamba ameamua kuelekeza juhudi zake katika kampeni za kumwezesha Dkt Ruto kuingia Ikulu mwaka huu.
“Mnamo Agosti mwaka huu wa 2022, sitatetea kiti changu cha Mumia Mashariki. Kwa hivyo, kwa heshima kuu nawaomba watu wa Mumias Mashariki kuchagua kiongozi ambaye ataboresha yale ambayo tumetekeleza pamoja. Mchague mtu mchapa kazi,” akasema kupitia akaunti yake ya Twitter
.Bw Washiali pia aliwashukuru wakazi wa eneo bunge hilo kwa kumpa nafasi ya kuwahudumia kwa miaka 15, tangu mwaka wa 2007 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kama mbunge ya iliyokuwa eneo bunge la Mumias.
Japo imesemekana kuwa huenda Bw Washiali akawania wadhifa wa useneta wa Kakamega, mbunge huyo amekana madai hayo na kushikilia kuwa hatawania kiti chochote cha kuchaguliwa.
Next article
Wanyonge maskini wanavyopuuzwa