Connect with us

General News

ODM sasa yapiga UDA chenga Kilifi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

ODM sasa yapiga UDA chenga Kilifi – Taifa Leo

ODM sasa yapiga UDA chenga Kilifi

NA MAUREEN ONGALA

CHAMA cha ODM kimeongeza matumaini ya kudhibiti ngome yake katika Kaunti ya Kilifi, baada ya wanasiasa waliokiasi kuanza kubadili misimamo yao.

Mwanasiasa wa hivi punde aliyekuwa ameasi chama hicho ambaye ameamua kurudi ni Mbunge wa Kaloleni, Bw Paul Katana.

Bw Katana, ambaye alikuwa akijihusisha na mrengo wa Naibu Rais William Ruto licha ya kuwa ni mwanachama wa ODM, alisema hataki kuhusishwa na chama kingine chochote kuelekea kwa uchaguzi ujao.

Kulingana naye, ukaribu wake na wanasiasa wapinzani wa ODM ulikuwa tu kwa minajili ya kuletea eneobunge lake maendeleo.

“Mgombeaji wa urais nitakayemuunga mkono ni Raila Odinga, na ninawaomba nyote muungane nami kumpigia debe ili achaguliwe ifikapo Agosti. Mimi nikiwa mbunge, ninakaribisha kiongozi wa mrengo wowote anayetaka kuja kusaidia watu wangu lakini hilo halitabadili msimamo wangu wa kisiasa,” akasema.

Alikuwa akihutubu katika Shule ya Msingi ya Mahenzo, wakati wa kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa madarasa yatakayogharimu Sh6.7 milioni.

Bw Katana alitoa tangazo hilo Jumatano wakati ambapo aliyekuwa Mbunge wa Magarini, Bw Harrison Kombe, pia alikuwa anakaribishwa rasmi chamani na Bw Odinga jijini Nairobi.

Bw Kombe ambaye alikuwa mbunge mwaka wa 2013 hadi 2017, alikuwa ni mwanachama wa United Republican Party (URP), ambacho kilikuwa chama tanzu cha Muungano wa Jubilee kilichoongozwa na Dkt Ruto.

Hayo yametokea wiki chache baada ya Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, pia kuamua kuunga mkono azimio la Bw Odinga kupitia kwa chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA).

Bw Kingi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa ODM Kilifi, aliasi chama hicho akaanza kupigania juhudi za kuunda chama kimoja cha Pwani. Juhudi hizo ziligonga mwamba viongozi wa vyama vya Pwani walipokataa kuvivunja.

Kati ya kaunti sita za Pwani, ODM ilitamba zaidi Kilifi katika uchaguzi wa 2017 , kwani wabunge wote wa maeneobunge saba waliwania kupitia chama hicho kando na gavana, seneta, mbunge mwakilishi wa wanawake na idadi kubwa ya madiwani.

Hata hivyo, ngome hiyo ya Bw Odinga ilitikiswa wakati baadhi ya wabunge walipoanza kuegemea upande wa Dkt Ruto, anayepanga kuwania urais kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA), wakiongozwa na Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Bw Kazungu Katana, ilitarajiwa wanasiasa wangeanza kubadili misimamo yao kadri na jinsi Uchaguzi Mkuu unavyokaribia.

Mwenyekiti wa chama hicho katika Kaunti ya Kilifi, Bw Teddy Mwambire, alisema amekuwa akijitahidi kushawishi walioasi ODM warudi na vilevile kutafuta wanachama wapya kutoka vyama vingine.

“Nilipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa ODM Kilifi niliomba nipewe siku 100 kufanya mabadiliko katika chama na nimetimiza kwa sababu kuna wanachama wengi wanarudi na wengine wapya pia wanaendelea kujiandikisha,” akasema.

Alisema ana matumaini wanasiasa wengine walioasi chama hicho watarudi kabla milango ifungwe kwani tarehe ya kura za mchujo inazidi kukaribia.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending