Maafisa wa kaunti wajiandaa kujiuzulu ili kuingia kwa siasa
NA LUCY MKANYIKA
WAFANYIKAZI katika Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta ambao wanataka kuwania viti vya kisiasa katika uchaguzi ujao, wameanza kujiandaa kujiuzulu kabla ya Februari 9.
Waziri wa Ardhi katika kaunti hiyo, Bw Mwandawiro Mghanga, tayari amewasilisha notisi ya kujiuzulu ili apate nafasi ya kuwania useneta.
Bw Mghanga, 63, amepanga kuwania cheo hicho kupitia chama cha Communist Party of Kenya ambacho yeye ndiye mwenyekiti.
Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Bw Mghanga alithibitisha kuwa tayari amewasilisha barua yake kwa Gavana Granton Samboja kumfahamisha angependa kujiuzulu ifikapo mwezi ujao.
“Bado niko kazini hadi mwezi ujao. Ninasubiri kipenga kipigwe kisha nianze kampeni rasmi,” akasema.
Mwanasiasa huyo amekuwa ulingoni kwa miaka mingi, na ni mmoja wa waliokamatwa mwaka wa 1985 kwa madai ya kupanga mapinduzi ya serikali ya aliyekuwa rais Daniel arap Moi.
Baada ya utawala wa Moi, Bw Mghanga alifanikiwa kuwa Mbunge wa Wundanyi kuanzia mwaka wa 2002 hadi 2007.
Aliwania useneta katika uchaguzi uliopita lakini akaibuka wa tatu baada ya Seneta Jones Mwaruma na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Bi Joyce Lay.
Anatarajiwa kuwania kiti hicho dhidi ya Bw Mwaruma, John Rugha, Nataniel Noti na Mike Banton.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Bi Esther Mwanyumba, pia anatarajiwa kujiuzulu ili kuwania wadhifa wa Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti hiyo.
Kufikia sasa, hakuna mwanasiasa mwingine ambaye ametangaza nia ya kuwania kiti hicho.
Maafisa wengine wa kaunti ambao wanatarajiwa kujiuzulu ili wawanie viti vya kisiasa ni Waziri wa Kilimo, Bw Davis Mwangoma, msaidizi wa kibinafsi wa gavana, Bw Wilfred Mwalimo, na Afisa Mkuu wa Kaunti, Bw Simon Mwachia ambao wote wanataka kuwania ubunge Wundanyi.
Mshauri wa kisiasa wa gavana, Bw Bigvai Mwailemi pia anatarajiwa kuwania kiti cha ubunge Voi.
Next article
TAHARIRI: Serikali iwasake wanaoendesha uuzaji haramu wa…