Connect with us

General News

Hofu ya wakazi kubomolewa nyumba yatanda barabara ikiwekwa lami – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Hofu ya wakazi kubomolewa nyumba yatanda barabara ikiwekwa lami – Taifa Leo

Hofu ya wakazi kubomolewa nyumba yatanda barabara ikiwekwa lami

NA SIAGO CECE

Wakazi wa Kwale sasa wanahofia kubomolewa nyumba zao huku serikali, kupitia mamalaka ya barabara za mjini (KURA) ikianza mradi wa kupanua na kuweka lami barabara mjini Ukunda.

Hii ni baada ya mamlaka hiyo kuwapa wakazi notisi ya mwezi mmoja kuondoa majengo yao na miti kutoka kwa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita tano. Barabara hiyo ya kutoka Markaz hadi Shamu, inatarajiwa kupunguza msongamano katika barabara kuu ya Likoni-Lungalunga.

Kulingana na mpimaji wa KURA Victor Obiko, itahitajika kuongezwa upana wa mita 15 pande zote. Hii inamaanisha kuwa wakazi ambao wamejenga nyumba, karibu na barabara hiyo watahitajika kuondoka.

Lakini wenyeji, katika mkutano kati yao na KURA jana, walisema kuwa wangependa kulipwa fidia kwa wote ambao mali yao itakuwa imeharibiwa.

“Hamwezi tu kutupa mwezi mmoja kuondoa jengo ambalo limekuwa na biashara kwa miaka zaidi ya kumi. Hii ni kutufilisisha sisi kama wakazi,” Mohammed Juma, mkazi wa wadi ya Bongwe/Gombato alisema.

Hata hivo, Mhandisi wa KURA Vivian Nyamwalo alisema kuwa majengo yanayotakiwa kubomolewa, pamoja na miti ni yale ambayo yanapatikana katika hifadhi ya barabara ambayo si shamba la mtu.

Aliwaomba wenyeji wa Bongwe kushirikiana nao huku akiahidi kuwa mkandarasi atawapa vijana kazi wakati ujenzi wa barabara utakapoanza rasmi.

Waziri wa Barabara Kwale Hemedi Mwabudzo aliwasihi wenyeji kukaribisha mradi huo kwani unatarajiwa kuleta maendeleo katika eneo lao.

“Uzuri wa barabara ni kuwa itaimarisha eneo hili, na kutakuwa na watu engi ambao wataanza biashara zao hapa. Hii barabara ikikamilika tunatarajia kuwa bei ya mashamba pia itapanda zaidi,” Bw Mwabudzo alisema.

Haya yanajiri huku wakazi wanaoishi katika barabara kuu ya Likoni kuelekea Lungalunga wakianzisha mchango wa kumlipa wakili anayewawakilisha kortini.

Hii ni baada ya mamlaka ya barabara kuu za kutaifa (Kenha) kutangaza kuwa itapanua barabara hiyo kwa mita kumi kila upande, jambo ambalo limewasikitisha wenyeji.

Hapo awali barabara hiyo ilipanuliwa kwa mita thelathini ikisababisha ubomoaji wa majengo zaidi ya mia moja.

Mwenyekiti wa waathriwa wa ubomoaji utakaotekelezwa na Kenha Kwale Hamisi Athman alisema ni waathiriwa zaidi ya elfu thelathini wanaotarajiwa kuchanga pesa ili kulipa wakili ada yake.

“Imebidi tuungane kama waathirika katika mkanda huu ili tuweze kutetea haki zetu . Hatukatai kuwa serikali inaleta maendeleo ila tunadai kuwa wakichukua sehemu zetu kama ardhi na nyumba watulipe fidia,” Bw Athman alisema.

Alisema ubomoaji huo utawaathiri pakubwa hasa kwa wale wanaoishi karibu na barabara.