Connect with us

General News

PAA yajipanga kudhibiti kaunti kura za Agosti – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

PAA yajipanga kudhibiti kaunti kura za Agosti – Taifa Leo

PAA yajipanga kudhibiti kaunti kura za Agosti

NA ALEX KALAMA

CHAMA cha Pamoja African Alliance (PAA), kinajitahidi kudhibiti bunge la Kaunti ya Kilifi baada ya uchaguzi ujao kwa kutafuta ushindi wa idadi kubwa ya madiwani na ugavana.

Hayo yamedhihirika baada ya madiwani wanaoegemea chama hicho kutangaza kuanzisha kampeni za kupigia debe ugavana na udiwani.

Madiwani hao wameshikilia msimamo kwamba hawataunga mkono wagombeaji viti vya maeneo watakaotumia vyama vingine katika uchaguzi ujao.

Chama hicho kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kinatarajiwa kumsimamisha wakili George Kithi kama mgombea wake wa ugavana ikiwa hatakuwa na mpinzani ndani ya chama.

Zaidi ya madiwani 20 wa bunge la Kaunti ya Kilifi walisema msimamo wao kumuunga mkono Bw Kithi umetokana na kuwa wanaamini atafanikisha miradi ya maendeleo kwa wakazi wa kaunti hiyo kupitia kwa PAA.

Wakiongozwa na Diwani wa Wadi ya Sokoni, Bw Gilbert Peru, walisema sasa wataanza kuingia mashinani kuanza kampeni za ugavana.

Walisema wanataka kutia bidii ili kuhakikisha pia wamepata idadi kubwa ya madiwani katika bunge la kaunti.

“Hii timu iko hapa wote tutarudi pale bungeni na wao. Kwa hivyo kama wewe huko hapa wewe unaenda nyumbani. Na tutakuja wadi yako tutachukua mwingine ambaye anaunga mkono PAA na anaunga mkono Bw Kithi na kuchukua nafasi yako,” akasema Bw Peru.

Naye naibu wa wengi katika bunge la kaunti hiyo, Bw Sammy Ndago, ambaye pia ni diwani wa wadi ya Shimo la Tewa, alisema Bw Kithi ndiye mwenye uwezo wa kulinda raslimali za serikali ya Kaunti ya Kilifi.

“Sisi hatuangalii upande mwingine, kwa sababu muda umeenda. Tunechora mipango yetu hapa ndani, tumemaliza mipango sasa tunakuja mashinani,” alisema Bw Ndago.

Chama hicho tayari kilitangaza kuwa kinaunga mkono azimio la Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kwa urais.

ODM ina wanasiasa kadhaa wanaomezea mate tikiti ya kuwania ugavana Kilifi akiwemo Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, na Naibu Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Saburi.

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, anatarajiwa kuwania kiti hicho kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto.