Wanajeshi Burkina Faso wamzuilia Rais Kabore
Na MASHIRIKA
OUAGADOUGOU, Burkina Faso
RAIS Roch Kabore wa Burkina Faso jana Jumatatu alikamatwa na kuwekwa kizuizini na wanajeshi waasi ambao wamekuwa wakimshinikiza kuondoka mamlakani, zilieleza ripoti.
Wanajeshi hao wamekuwa wakimshinikiza kiongozi huyo kuwafuta kazi baadhi ya wakuu wao, na kutenga fedha zaidi kwenye harakati za kukabiliana na wapinagaji wa Kiislamu.
Ripoti zilisema milio ya risasi ilisikika karibu na Ikulu na makao makuu ya jeshi katika jiji kuu la Ouagadougou, usiku wa kuamkia Jumatatu.
Ripoti zilieleza baada ya kukamatwa, rais huyo alizuiliwa na wanajeshi hao katika kambi moja ya kijeshi.
Wanajeshi pia walizunguka makao makuu ya kituo cha televisheni cha serikali.
Mara tu baada ya hatua hiyo, mamia ya raia walijitokeza kuwaunga mkono, licha ya kafyu ambayo imewekwa na serikali.
Raia wenye ghadhabu pia walichoma makao makuu ya chama tawala.
Jumapili, vikosi vya usalama viliwarushia vitoa machozi mamia ya waandamanaji waliojitokeza jijini Ouagadougou kulalamikia hatua ya serikali kushindwa kukabili mashambulio ambayo yamekuwa yakitekelezwa na wapiganaji wa Kiislamu.
Waandamanaji hao walikuwa wakitoa matamshi ya kumkashifu Rais Kabore, wakimtaka kujiuzulu mara moja.
“Wapiganaji hao wanafanya mashambulio karibu kila sehemu ya nchi. Mamia ya watu wanauawa huku wengine wakitoroka makwao. Tunamtaka Kabore na serikali yake kujiuzulu kwani hali ya nchi si nzuri hata kidogo. Hatutawaunga mkono hata kidogo,” akasema Amidou Tiemtore, aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji hao.
Baadhi ya waandamanaji pia walieleza kuiunga mkono Mali, ambao raia wake wameeleza kukasirishwa na hatua ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kuiwekea nchi yao vikwazo. ECOWAS ilichukua hatua hiyo kama adhabu ya utawala wa jeshi la Mali kukosa kubuni serikali ya mpito, kulingana na mwafaka uliofikiwa kati ya pande hizo mbili.
Maasi hayo nchini Burkina Faso yanajiri huku mamia ya raia wake wakiendelea kuuawa kwenye mashambulio yanayotekelezwa na wanamgambo wanaodaiwa kuwa na uhusiano na makundi ya kigaidi ya Al-Qeeda na Islamic State (IS).
Kufikia sasa, maelfu ya watu wameuawa huku wengine zaidi ya 1.5 milioni wakiachwa bila makao.
Kulingana na Umoja wa Mataifa (UN), karibu watu 12,000 walifurushwa kutoka makwao katika muda wa wiki mbili pekee mwezi Desemba.
Wanajeshi wanne wa Ufaransa pia walijeruhiwa kwenye operesheni ya pamoja waliyoendesha na wenzao wa Burkina Faso.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa wanajeshi wa Ufaransa kujeruhiwa tangu 2019, wakati wanaume wawili waliuawa kwenye operesheni ya kuwaokoa mateka kadhaa waliokuwa wakishikikiwa na wanamgambo.
Ufaransa ina jumla ya wanajeshi 5,000 katika eneo la Afrika Magharibi.
Wanajeshi hao hawajakuwa wakiingilia sana masuala ya ndani ya Burkina Faso, ikilinganishwa na Niger ama Mali.
Hii ni mara ya pili kwa serikali ya Rais Kabore kuwakabili waandamanaji tangu Novemba.
Maandamano hayo yanajiri baada ya serikali hiyo kufunga mtandao wa Facebook wiki iliyopita, ikieleza kuchukua hatua hizo kutokana na sababu za kiusalama.
Vile vile, iliwakamata watu 15 kwa tuhuma za kupanga njama za kuipindua kutoka uongozini.
Desemba 2021, kiongozi huyo alimfuta kazi waziri mkuu na kuwateua mawaziri wapya.
Kabla ya kukamatwa kwake jana, duru zilieleza vikosi vya usalama vilikuwa vikipanga kufanya mashauriano na wanamgambo hao.
Hata hivyo, raia wanasema huenda mazungumzo hayo yakakosa kuzaa matunda yoyote, kwani yatazua taswira ya serikali imeshindwa kuidhibiti nchi.