Hofu mapinduzi yakizuka upya Afrika Magharibi
Na MASHIRIKA
OUAGADOUGOU, Burkina Faso
KUFUATIA mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso, Jumatatu, ambapo wanajeshi waasi walimng’oa mamlakani Rais Roch Kabore, wadadisi wanasema eneo la Afrika Magharibi sasa linashuhudia wimbi jipya la mapinduzi.
Hili ni licha ya mataifa mengi katika eneo hilo kuonekana kuanza kukumbatia mfumo wa kidemokrasia.
Kufikia sasa, nchi tatu kati ya kumi ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), zinatawaliwa na wanajeshi.
Nchi hizo ni Burkina Faso, Mali na Guinea.
Mapinduzi ya Burkina Faso yanatokea miezi mitano tu baada ya wanajeshi waasi kumpindua Rais Alpha Conde wa Guinea.
Hili pia ni baada ya mapinduzi mawili yaliyofanyika Mali Agosti 2020 na Mei mwaka uliopita mtawalia, ambapo wanajeshi walimng’oa mamlakani Rais Boubacar Keita.
Baada ya mapinduzi hayo, wanajeshi waliiahidi ECOWAS kwamba wangeandaa uchaguzi mkuu kufikia mwezi uliofuata, lakini hawakutimiza hilo.
Mapinduzi ya Mei 2021 yalitajwa kuhujumu mchakato mzima wa kubuni serikali ya mpito.
Badala yake, walisema watakaa mamlakani kwa miaka mitano, wakishikilia “ni baada ya muda huo pekee ambapo watafanikiwa kubuni serikali hiyo.”
Kinaya ni kuwa, mapinduzi hayo yanatokea katika eneo ambako demokrasia ilionekana kukumbatiwa na nchi nyingi.
Kuna uwezekano enzi ya mapinduzi ya kijeshi imeanza kurejea eneo hilo?
Kulingana na mdadisi wa siasa za Afrika Magharibi, Paul Melly, kuna dalili mapinduzi hayo yanaashiria urejeo wa mapinduzi hayo.
“Hizi ni dalili mpya enzi hiyo inarejea. Itakuwa athari mbaya ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa kudhibiti maasi hayo,” akasema.
Hata hivyo, anawalaumu baadhi ya viongozi kuwa chanzo cha mapinduzi hayo.
Nchini Guinea, Rais Conde analaumiwa kuchangia mapinduzi yaliyotokea huko.
Rais Conde alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama rais mnamo 2010, japo akageuka na kuwa dikteta, kwa kubadilisha katiba ili kumruhusu kuwania urais.
kwa kipindi cha tatu mnamo 2010.
Vile vile, aliwafunga gerezani baadhi ya watu waliojitokeza kumkosoa kutokana na utawala wake.
Alipopinduliwa mamlakani Septemba mwaka uliopita, raia wengi wa taifa hilo walifurahia mapinduzi yake kutokana na mateso yaliyoendeshwa na utawala wake.
Chama chake cha kisiasa pia kilionekana kuunga mkono mapinduzi yake.
Kinyume na Burkina Faso, hali ni tofauti nchini Mali, kwani mapinduzi yamechangiwa na changamoto za kiusalama.
Raia wamekuwa wakiikosoa serikali kwa kushindwa kuwakabili wanamgambo wa Kiislamu ambao wamekuwa wakifanya mashambulizi katika sehemu tofauti.
Wanajeshi pia walikuwa wakilalamikia serikali kwa kutowalipa vizuri na kutowapa silaha nzuri, ikilinganishwa na wanamgambo hao.
Wadadisi wanasema kuwa kama Mali, mapinduzi ya Burkina Faso yamesababishwa kwa upande mmoja na wanajeshi wanaohisi serikali ilikuwa ikiwatuma katika maeneo ya vita bila kushughulikia maslahi yao ifaavyo.
Ripoti zilisema wanajeshi wengi walihisi serikali haikuwa ikiwajali baada ya wanamgambo waliojihami vikali kushambulia kambi ya kijeshi ya Inata, kaskazini mwa taifa hilo, ambapo wanajeshi 53 waliuawa. Kambi hiyo ilikuwa na wanajeshi 120.
Baada ya mapinduzi hayo, Rais Kabore alianza kushinikizwa kufanya mageuzi katika idara za usalama nchini humo.
Kiongozi huyo alifanya mageuzi ya kwanza katika idara kadhaa likiwemo jeshi, kwenye juhudi za kurejesha uthabiti wa kisiasa katika mikoa ya kaskazini na mashariki.
Kwa miaka miwili iliyopita, zaidi ya shule 1,000 zimefungwa huku watu zaidi ya 1.5 milioni wakitoroka kutoka makazi yao. Zaidi ya watu 2,000 wameuawa kwenye mapigano hayo.
Next article
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tunaomba Mola atufikishe mwezi…