KIGODA CHA PWANI: PAA yayumba kuhusu itakayeunga kwa urais
NA PHILIP MUYANGA
JE, msimamo wa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kuhusiana na uungaji mkono wa wagombeaji wa urais ni upi?
Chama cha PAA kimekuwa kikitoa kauli zionekanazo kukinzana, swala ambalo linaonekana kuwakanganya wafuasi wake na wapiga kura Pwani.
Takriban wiki mbili zilizopita viongozi wanaohusishwa na chama hicho wamekuwa wakitoa matamshi ambayo yanaashiria njia tofauti PAA inachukua kuhusiana na uungwaji mkono wa wagombeaji wa urais.
Katika mkutano wa kinara wa ODM Raila Odinga mjini Naivasha mnamo Januari 17, kiongozi wa PAA ambaye ni gavana wa Kilifi Amason Kingi pamoja na baadhi ya magavana wengine walisema kuwa wanamuunga mkono Bw Odinga kuchaguliwa kuwa rais.
Bw Kingi alisema kuwa ugatuzi utakuwa imara katika mikono ya Bw Odinga iwapo atachaguliwa kuwa rais wa nchi kuliko mgombeaji mwingine.
“Sisi kama magavana kupitia mwavuli wa Azimio la Umoja, tumekubaliana tukirudi mashinani gavana baada ya gavana tutaweka mikakati katika kaunti zetu kuona kwamba tunazungumza na kuhamasisha umma katika kaunti zetu,” alisema Bw Kingi.
Bw Kingi alisema kuwa anayeweza kupeleka gurudumu la ugatuzi na kuufanya usiyumbe ni Bw Odinga.
Kauli hii inaonekana kutofautiana na ile ya aliyekuwa mbunge wa Malindi Lucas Maitha aliyesema kuwa chama cha PAA kitaunga mkono mgombea wa urais ambaye atatimiza masharti ya wananchi wa Pwani.
Bw Maitha, ambaye ni mfuasi wa PAA, akihudhuria mkutano katika hoteli moja mjini Mombasa alisema kuwa iwapo Bw Odinga na kiongozi wa United Democratic Alliance (UDA) William Ruto wanataka kura za wapwani, basi lazima watimize matakwa yao.
Alisema kuwa iwapo wote hao wawili hawatakubali matakwa yao wataungana na kumpatia mgombeaji mwingine kura hata kama sio maarufu.
“Iwapo Raila anataka kura zetu basi aje na aongee na sisi, kura za urais zitatoka kwa masharti,” alisema Bw Maitha.
Bw Maitha aliongeza kusema kuwa mgombeaji yeyote atakayetimiza masharti ya watu wa Pwani basi watamuunga mkono.
Kauli hiyo iliungwa mkono na aliyekuwa mbuge wa Mwatate Bw Calist Mwatela aliyesema kuwa kwa miaka mingi eneo la Pwani limekuwa likiwa bila mwelekeo wa kisiasa.
Aliongeza kusema kuwa Pwani inachangia pakubwa uchumi wa nchi ndiposa wanataka kiongozi atakaye fanya kazi na jamii za Pwani lazima ahakikishe uchumi umezingatiwa na kwamba chama cha PAA hakihusiki na viti vya kisiasa tu bali maendeleo ya Pwani.
Kauli ya Bw Maitha na Bw Mwatela,inalingana na maafikiano ya Disemba 2021 ambapo katika mkutano wa chama hicho iliafikiwa ya kuwa wanachama wataunga mkono mrengo ambao utasikiliza mahitaji yao na kukubali kuyatekeleza unapotwaa uongozi wa nchi.
Wakati wa mkutano huo wa PAA mwaka jana,Bw Kingi alisema kuwa kila kona ya nchi watu wanajipanga na kwamba wakati wa eneo la pwani wa kujipanga ni sasa.
“Tumezoea kupangwa, wakati kwa sasa umefika tujipange sisi wenyewe,” alisema Bw Kingi wakati wa mkutano huo ulikuwa umehudhuriwa na viongozi wa zamani wa kisiasa kutoka maeneo tofauti tofauti ya pwani.
Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa, kauli tofauti za chama cha PAA zinaonyesha ya kuwa hakijakuwa na msimamo thabiti iwapo watamuunga mkono Bw Odinga au Bw Ruto.
Wachanganuzi wa kisiasa wanatofautiana kuhusiana na ishara ya chama cha PAA ya kuonekana kutokuwa na msimamo thabiti.
Baadhi yao wanasema kuwa chama cha PAA kwa kuwa hakina mgombeaji wa urais kinafaa kuwaacha wafuasi wake kuamua wenyewe ni mgombeaji yupi wa urais ambaye watamchagua.
Hata hivyo wengine wanasema kuwa ni vyema kwa chama hicho ambacho asili yake ni ya Pwani kutoa msimamo kamili na kusema ni mrengo upi ambao wanataka wafuasi wao waufuate.
Mchanganuzi wa siasa Bi Maimuna Mwidau alisema matamshi ya viongozi hao wawili yanamaanisha ya kuwa hawataunga mkono mgombeaji yeyote wa urais bila mpangilio wowote.
“Wanapima ni kipi watapata kwa faida ya wananchi wa Pwani kwa kuwa kuna maswala ya kipekee ambayo yanaathiri Pwani,kama vile ardhi,” alisema Bi Mwidau.
Bi Mwidau aliongeza kusema kuwa kulingana na viongozi hao kila mogobeaji urais lazima aseme wazi ni swala gani atakalowafanyia wakaazi wa Pwani.
Aliyekuwa afisa wa chama cha KANU mjini Mombasa hapo zamani Bw Abdulrahman Abdallah anasema kuwa inafaa PAA kuwa na msimamo mmoja ambao wafuasi wao watauunga mkono.
“Kama PAA haina kauli moja basi itawezaje kushawishi watu kupigia au kuunga mkono mwaniaji wa urais?” aliuliza Bw Abdallah.
Bw Abdallah alisema kuwa kutokuwa na kauli moja kunaweza pia kumaanisha ya kuwa Bw Kingi alikuwa anaunga Azimio la Umoja yeye binansfi na sio kama chama cha PAA.
Makao makuu ya Pamoja African Alliance jijini Mombasa. PICHA | MAKTABA
Hata hivyo mchanganuzi mwingine wa siasa aliyetaka jina lake libanwe alisema kuwa kwa sasa chama cha PAA kinafaa kuwaacha wafuasi wake kuunga mkono wagombeaji urais ambao wanataka.
“PAA haisimamishi mgombeaji urais yeyote, kwanini wasema kuwa watapeana masharti ya uungwaji mkono?” alisema mdadisi huyo.
Chama cha PAA ni mojawapo ya vyama asilia vya Pwani ambavyo vinasema kuwa malengo yake ni kuimarisha maisha ya wakaazi kiuchumi, kisiasa na maendeleo.
Vyama vingine ni Shirikisho Party of Kenya, Umoja Summit Party, Kadu Asili na Republican Congress Party.
Kulingana na wachanganuzi wa siasa kutoimarika kwa vyama vya kisiasa vya eneo la Pwani kunasababishwa na ukosefu wa fedha na wafadhili ambao huhakikisha utenda kazi wa chama unatekelezwa.