Wito polisi wajengewe vituo vya ushauri nasaha
OSCAR KAKAI NA CHARLES WASONGA
SERIKALI imetakiwa kubuni vituo vya kutoa ushauri nasaha na mafunzo ya kidini katika ngazi za kaunti ndogo na wadi kote nchini ili kudhibiti kero la matatizo ya kiakili miongoni mwa maafisa wa polisi.
Hiyo itakuwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha maslahi ya maafisa hao kote nchini kupitia ushauri nasaha na usaidizi wa kisaikolojia.
Mpango huo pia utachangia kupunguzwa kwa visa vingi vya mauaji miongoni mwa maafisa hao ambavyo vimekuwa vikiongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
Pendekezo hili lilitolewa Jumapili na maafisa wa polisi katika hafla ya kipekee ambapo afisa mmoja wa polisi aliyestaafu aliwaalika marafiki na majirani kusherehekea miaka 42 aliyohudumu katika idara ya polisi.
Afisa huyo wa zamani John Arile aliandaa sherehe hiyo nyumbani kwake katika kijiji cha Kusolol eneo la Chepareria, kaunti ya Pokot Magharibi.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na maafisa kadha wa polisi waliostaafu pamoja na wale wanaohudumu wakati huu.
Bw Arile alisema kwa mujibu wa tajriba yake katika idara ya polisi, visa vya polisi kujiua au kuua wenzao husababishwa na utovu wa nidhamu, matumizi ya mihadarati na unywaji pombe kupita kiasi.
“Huduma ya Kitaifa ya Polisi inafaa kutoa ushauri na usaidizi wa kisaikolojia kwa maafisa wa polisi ili kuimarisha maisha yao wakiwa kazini. Ni muhimu kuzingatia kuwa baadhi ya maafisa wamepotoka kinidhamu kutokana na historia ya familia zao,” akasema.
“Hii ndio maana napendekeza kwamba vituo maalum vya kutoa ushauri nasaha kwa maafisa wa polisi vianzishwe hadi katika ngazi ya wadi ili kuwasaidia maafisa hawa. Wataalamu katika nyanja za ushauri nasaha, saikolojia na mafunzo ya kidini waajiriwe kuhudumu katika vituo hivi,” Bw Arile akasema.
Alisema baadhi ya maafisa wa polisi hujiua kutokana na msongo wa kiakili na matatizo mengine ya kimawazo.
Aliongeza kuwa mauaji mengine yanatokana na msongo wa kiakili unatokana na matatizo kazini, utovu wa mawasiliano kati ya wakuu wa polisi na wadogo.
“Mafisa wa polisi hukumbwa na changamoto nyingi za kikazi. Kwa mfano, afisa anaweza kuhamishwa hadi maeneo yenye mazingira magumu ya kikazi, na hivyo kutenganishwa na watoto wake wanasoma. Maafisa kama hawa wanafaa kushauriwa kwamba hii isiwe sababu ya wao kujitoa uhai,” Bw Arile akasema.
Kulingana na ripoti iliyotolewana Tume ya Huduma ya Kitaifa za Polisi (NPSC) wiki jana jumla ya maafisa 12, 000 wanakabiliwa na matatizo ya afya ya kiakili nchini.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni ulibaini kuwa kati ya asilimia 12 na asilimia 13 ya maafisa wa polisi 110,000 nchini wanazongwa na matatizo ya kiakili.
Afisa Mkuu Mtendaji wa NPSC Joseph Onyango alisema takwimu hizo zinaakisi hali ya changamoto hiyo ulimwenguni.
“Visa vya matatizo ya kiakili miongoni mwa maafisa wa polisi nchini vimefikia kiwango cha kati ya asilimia 12 na asilimia 13 ya idadi jumla ya maafisa wa polisi nchini. Kiwango hiki kinakaribia kile cha ulimwenguni,” akasema.
Bw Onyango alisema tume hiyo imeelekeza juhudi na rasilimali katika mpango wa kupambana na jinamizi hili ambalo linaathiri utendakazi wa maafisa wa polisi.