Gicheru ataka ICC isiidhinishe nakala
NA VALENTINE OBARA
WAKILI Paul Gicheru, ameitaka Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC), isiruhusu upande wa mashtaka kutumia nakala za mahojiano aliyofanyiwa awali na wapelelezi wa mahakama hiyo.
Upande wa mashtaka ulikuwa umedai kuwa, katika mahojiano hayo, Bw Gicheru alikiri kusaidia mashahidi kujiondoa katika kesi iliyomwandama Naibu Rais William Ruto, kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.
Kupitia kwa Bw Michael Karnavas ambaye ndiye wakili wake, Bw Gicheru sasa amesema atakuwa hatendewi haki iwapo upande wa mashtaka utakubaliwa kutumia nakala hizo kama ushahidi dhidi yake.
Ingawa amekiri kuwa alisaidia mashahidi kuandaa hati za kisheria kubatilisha ushirikiano wao na ICC, amesisitiza hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha alifanya hivyo kwa kusudi la kuwaondoa katika kesi ya Dkt Ruto, ambaye alikuwa ameshtakiwa pamoja na mwanahabari Joshua Sang.
“Hati ambazo Bw Gicheru alimwandalia shahidi P-0015 hazithibitishi kuwa “mshtakiwa alihusika moja kwa moja kupanga mashahidi wa upande wa mashtaka wajiondoe kutoka kwa kesi ya Ruto na Sang”. Zinathibitisha tu kuwa, Bw Gicheru aliandaa hati kwa niaba ya shahidi P-0015 ili ajiondoe ICC,” akasema.
Bw Gicheru pia alikanusha madai ya upande wa mashtaka kwamba alipohojiwa alisema alisoma katika Shule ya Upili ya Kapsabet pamoja na Dkt Ruto.
Hivi majuzi, kiongozi wa mashtaka aliwasilisha ombi kutaka Jaji Miatta Maria Samba, anayesikiliza kesi ya Bw Gicheru, kuruhusu nakala za mahojiano hayo aliyofanyiwa mwaka wa 2018 na maafisa wa ICC, zitumiwe kama ushahidi dhidi yake.
Nakala hizo zilidai kuwa, Bw Gicheru alikiri kushirikiana na watu wengine akiwemo marehemu Meshack Yebei, kuwasaidia mashahidi kuandika hati za kisheria za kujiondoa kwa kesi ya Dkt Ruto.
Bw Yebei alipatikana ameuawa na mwili wake kutupwa katika mbuga ya wanyamapori ya Tsavo, eneo la Voi mnamo Januari 2015, baada ya kutekwa nyara Eldoret mnamo Desemba 2014.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Bw James Stewart, umekuwa ukitafuta aina nyingine za ushahidi kwa muda sasa ili kuthibitisha wakili huyo alivunja sheria za kimataifa kwa kusaidia kulemaza kesi kuhusu uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Hii ni baada ya kubainika kuwa baadhi ya mashahidi ambao wangetegemewa katika kesi hiyo, wamekataa kushirikiana na mahakama.
Mbinu hizo zinajumuisha kutumia nakala za mahojiano ambayo mashahidi hao walifanyiwa awali kabla kukomesha mawasiliano na maafisa wa upande wa mashtaka wa ICC, zikiwemo video.
Juhudi za upande wa mashtaka kutaka nchi ambapo mashahidi hao wamesitiriwa zisaidie kuwafikisha mahakamani, hazijafua dafu.
Wengine wao ni wale wale waliokuwa wakitegemewa katika kesi ya naibu rais, na walipelekwa mafichoni kwa vile iliaminika usalama wao, ungekuwa hatarini iwapo ingejulikana mahali ambapo wanaishi pamoja na familia zao.
Ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 zilisababisha mauaji ya zaidi ya watu 1,000 huku maelfu wengine wakipoteza makao yao, na wengine wengi wakiachwa na majeraha ya kudumu.