Afueni kwa wauguzi serikali ikizindua mpango maalum wa mafunzo ya Kiingereza
Na MARY WANGARI
WAUGUZI kutoka Kenya wenye ndoto ya kufanya kazi katika mataifa ya kigeni wana sababu ya kutabasamu baada ya serikali kuzindua mpango maalum wa mafunzo ya Kiingereza.
Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo uliofanyika katika Makao Makuu ya Chuo cha Mafunzo kuhusu Utabibu, Jumanne, Februari 1, 2022, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema mpango huo utaboresha umilisi wa Kiingereza miongoni mwa wauguzi nchini.
Aidha, alifafanua kuwa kupitia mpango huo ambao ni wa kwanza wa aina yake nchini, serikali inalenga kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi unaotimiza viwango vya kimataifa kuhusiana na mkataba uliotiwa saini majuzi kati ya Kenya na Uingereza.
“Hafla hii ni ya kihistoria kwa kuwa ndiyo mara ya kwanza kabisa kwa serikali kuanzisha mpango kama huu wa mafunzo ambapo tutawapiga msasa vijana wetu kupokea mafunzo ulaya,”
“Lengo letu ni kuwa na kikosi cha wafanyakazi waliofuzu kimataifa na walio na ujuzi unaohitajika ndiposa tunajivunia hili. Ni muhimu kuwa Wakenya wanaweza kusafiri Uingereza bila kujificha au kujihisi kama wakimbizi bali wawe wakisafiri kama wageni wanaoheshimiwa,” alisema Dkt Kagwe.
Kuhusiana na madai kuwa wauguzi kutoka Kenya hawafahamu Kiingereza, Dkt Kagwe alikuwa na wakati mgumu kufafanua hali hiyo na wakati huo huo akisisitiza umuhimu wa mradi huo katika kuwapa wahudumu wa afya ujuzi unaohitajika kupasi mitihani ya kitaifa.
“Sikusema hatuwezi kuzungumza Kiingereza. Tunaweza kuzungumza kimombo bora sana ndiposa tunaweza kufunza somo hilo katika mataifa mengine. Hata hivyo, hii haimaanishi tutapita mitihani ya kitaaluma inayohitajika katika soko la kimataifa,” alifafanua.
Kulingana na Dkt Kagwe, mradi huo vilevile utajumuisha lugha nyinginezo huku Kenya ikiendelea kutuma wafanyakazi zaidi Ulaya katika mataifa yaliyotia saini mkataba na serikali ya Kenya.
“Haitakuwa Kiingereza. Kundi hilo lingine litatumwa katika mataifa mbalimbali ikiwemo Kuwait ambayo imeagiza manesi 598, Saudi Arabia ambayo tuna mkataba nayo miongoni mwa nchi nyinginezo,” alisema.
Kagwe aliipongeza serikali ya Uingereza kwa ushirikiano huo unaolenga kunufaisha vijana zaidi ya 12,000 wanaosomea taaluma ya matibabu na wanaofuzu kila mwaka kutoka vyuo vikuu na vyuo vya mafunzo.