OKA watafuta ‘Bwana Harusi’
Na WANDERI KAMAU
MUUNGANO wa Okoa Kenya Alliance (OKA) umejitokeza kuwa utakaoamua mshindi kwenye kinyang’anyiro cha urais hapo Agosti 9, baada ya vinara wake kutia saini mwafaka wa ushirikiano Jumatano.
Muungano huo unawashirikisha kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Seneta Gideon Moi (Kanu), Bi Martha Karua (Narc-Kenya) na mwanasiasa Cyrus Jirongo wa United Democratic Party (UDP).
Mara tu baada ya kutia saini mwafaka huo, Bw Musyoka alisema wameombwa na baadhi ya mirengo ya kisiasa kujiunga nayo, japo watafanya hivyo “baada ya kushauriana kwa kina.”
“Tumeomba na mirengo kadhaa tuungane nao. Hata hivyo, tunataka mazungumzo hayo kuwa wazi. Hilo ni baada ya vyama vyote wanachama wa OKA kushauriana na kulewana,” akasema Bw Musyoka.
Awali, muungano huo uliwashirikisha pia Musalia Mudavadi (ANC) na Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya), kabla yao kuhama na kujiunga na mrengo wa Naibu Rais William Ruto, anayeongoza chama United Democratic Alliance (UDA). Watatu hao wametangaza kubuni muungano wa Kenya Kwanza Alliance (KKA), ambapo Dkt Ruto ndiye atakuwa mgombea urais wake.
Ikizingatiwa sasa ushindani mkuu wa kisiasa uliopo unaonekana kuwa kati ya Kenya Kwanza na vuguvuvu la Azimio la Umoja linaloongozwa na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, wadadisi wanasema ni wazi OKA ndiyo itakayoamua mrengo utakaoibuka mshindi.
“Ni wazi kuna uwezekano mkubwa OKA ndio watakaoamua mshindi kwenye uchaguzi wa urais Agosti. Hii ni ikizingatiwa kuwa ikiwa watamteua mmoja wao kuwania urais, basi atagawanya kura, hivyo kuinyima miungano ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja ushindi wa moja kwa moja,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.Kulingana na Katiba, lazima anayetangazwa kuwa mshindi wa urais kupata angaa asilimia 50 ya kura.
UMAARUFU MDOGO
Wadadisi wanasema ijapokuwa Bw Odinga na Dkt Ruto ndio wanaonekana kuwa washindani wakuu, tofauti ya umaarufu wao ni ndogo sana.
“Wingi wa wapigakura katika ngome za vigogo hao wawili ni kama unatoshana. Hivyo, itawalazimu kutafuta washirika zaidi wa kisiasa ili kuongeza kura kwenye vikapu vyao,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa.
Kwenye matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2017 (kabla ya muungano wa NASA kususia duru ya pili ya uchaguzi), Rais Kenyatta alizoa asilimia 54.1 ya kura huku Bw Odinga akipata asilimia 44.9.
Wadadisi wanataja tofauti hiyo kuwa ndogo sana, kwani Bw Odinga ameanza kupenya kisiasa katika maeneo yanayoonekana kuwa ngome za Dkt Ruto, kama vile Mlima Kenya.
Suala jingine linalotajwa kuupa muungano wa OKA nguvu licha ya kuonekana kuwa dhaifu kisiasa ikilinganishwa na Azimio na Kenya Kwanza, ni ushawishi wa kisiasa wa Bw Musyoka katika eneo la Ukambani.
Wadadisi wanasema ikiwa Bw Musyoka atapeperusha bendera ya muungano huo kwenye kivumbi cha urais, basi inamaanisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wenyeji wa Ukambani watamuunga mkono kama ilivyokuwa 2007.
Kulingana na takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), eneo la Ukambani lina karibu kura milioni mbili.
Ijapokuwa Bw Musyoka anakabiliwa na upinzani kutoka kwa magavana Charity Ngilu (Kitui), Prof Kivutha Kibwana (Makueni) na Dkt Alred Mutua (Machakos), wadadisi wanamtaja kuwa kigogo ambaye bado ushawishi wake wa kisiasa ni mkubwa Ukambani.
Next article
Mkewe Joho aomba talaka