Raila asema ukombozi wa tatu na wa kufufua uchumi umeanza
NA SAMMY WAWERU
KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga Jumatano aliendeleza kampeni zake kusaka kura kuingia Ikulu katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
Bw Odinga alifanya misururu ya kampeni katika Kaunti ya Kajiado, ambapo alitumia jukwaa hilo kuwarai Wakenya kumchagua kuwa rais akihoji shabaha yake ni kukomboa uchumi.
Waziri huyo Mkuu wa zamani, aidha alirejelea historia ya Kenya, kuanzia ukombozi wa taifa na kupitishwa kwa Katiba ya sasa – iliyozinduliwa 2010.
“Mimi ndiye nitaongoza oparesheni ya tatu kukomboa Kenya, ambayo ni ukombozi wa uchumi,” Bw Odinga akasema, akihutubia umati eneo la Kitengela.
Kiongozi huyo wa upinzani anayeshirikiana kwa karibu na Rais Uhuru Kenyatta, baada ya wawili hao kutangaza kuzika tofauti zao za kisiasa Machi 2018 kupitia mapatano ya Handisheki, alisema lengo lake ni vijana katika kukomboa uchumi.
“Sisi kama Wakenya tuna sababu na uwezo kubadilisha uchumi,” akasisitiza.
Akiuza sera zake kumrithi Rais Kenyatta, alisema vita dhidi ya ufisadi, ubadhirifu wa mali ya umma na matumizi mabaya ya ofisi ni miongoni mwa vigezo atakavyovipa kipau mbele.
“Adui wengine ni ugonjwa, ujinga, na umaskini.”
“Hawa ndio adui wa Kenya na Baba yuko tayari mstari wa mbele kupambana nao,” akasema.
Kufuatia ahadi chungu nzima anazotoa chini ya vuguvugu la Azimio la Umoja, Bw Odinga alisema anafahamu bayana atakapotoa pesa kuafikia miradi yake ya maendeleo.
“Nimeskia wengine wakisema ati oohh Baba anadanganya Wakenya, hakuna pesa. Baba hawezi akadanganya. Mimi Raila Amollo Odinga nilikuwa Waziri Mkuu, ninajua ziliko fedha. Nitaziba mianya yote ya ufisadi,” akafafanua.
Bw Odinga, alihudumu kama Waziri Mkuu chini ya utawala wa serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais (mstaafu) Mwai Kibaki.
Akielekeza makombora yake ya cheche za kisiasa kwa naibu wa rais, Dkt William Ruto, aliahidi chini ya utawala wake masomo kuanzia chekechea hadi chuo kikuu hayatatozwa karo.
“Vijana wakihitimu, wapate kazi ya maana ila si ya kusukuma wilibaro,” akaahidi.
Bw Odinga alikuwa ameandamana na Gavana wa Kajiado, Joseph Ole Lenku, Hassan Joho (Mombasa), aliyekuwa mgombea wa ugavana Nairobi, Bw Peter Kenneth, mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, kati ya viongozi na wanasiasa wengine.
Next article
OKA watafuta ‘Bwana Harusi’