Viongozi wa PAA waganda kwa Raila
NA BRIAN OCHARO
CHAMA cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachohusishwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi, kimepiga hatua katika juhudi zake za kutaka kujiunga rasmi na Muungano wa Azimio La Umoja.
Chama hicho Ijumaa kilitangaza katika makao yake makuu mjini Mombasa kwamba wanachama na uongozi wake sasa wamekubali kwa kauli moja kujiunga na vuguvugu hilo linaloongozwa na Bw Odinga kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8.
Tangazo hilo lilitolewa kufuatia mkutano wa takriban saa tatu uliohudhuriwa na viongozi wakuu wa chama hicho na zaidi ya wawaniaji 200.
Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama hicho, Bw Lucas Maitha alisema mazungumzo yako katika hatua ya juu zaidi ili kujiunga rasmi na vuguvugu hilo katika maandalizi ya kuandaa kampeni za Bw Odinga.
“Hivi karibuni tutatangaza habari za mapatano ya chama na vuguvugu la Azimio La Umoja kisha tujiunge nalo,” alisema Bw Maitha.
Kwa mujibu wa uongozi wa chama hicho, Bw Odinga ndiye aliyeanzisha mazungumzo hayo ambayo yatapelekea chama hicho kujiunga rasmi na vuguvugu hilo.
“Hatutavunja chama chetu bali tutajiunga na vuguvugu hilo. Uongozi wa chama bado utaendelea kuwa hivyo,” mwenyekiti huyo alisema.
Mgombeaji ugavana kaunti ya Kilifi George Kithi alisema PAA ni chama cha kitaifa na akapongeza uamuzi wake wa kujiunga na vuguvugu la Azimio La Umoja alilolitaja kama timu itakayoshinda uchaguzi wa Agosti.
“PAA si chama cha Bw Kingi bali ni chama cha kitaifa ambacho kinalenga kuendeleza ajenda za watu wa Pwani,” akasema.
PAA imempa Bw Odinga orodha ya matakwa ambayo inataka yatimizwe.
Wanataka hakikisho kuwa Bw Odinga atarejesha kikamilifu huduma za bandari ya Mombasa ambazo wanadai zimehamishwa Nairobi na Naivasha na kufufua uchumi wa eneo hilo.
‘Tunamtaka Bw Odinga atuhakikishie kwamba agizo la kuhamisha shughuli za bandari hadi maeneo mengine litafutiliwa mbali ndani ya siku 100 za uongozi wake,” akasema.
Chama hicho pia kimesema kinamtaka Bw Odinga kuwahakikishia kwa njia ya maandishi kuwa serikali yake itaanzisha mfuko wa makazi ya maskwota ili kutokomeza tatizo la maskwota katika ukanda wa Pwani
Wanasiasa wa Pwani wanaounga mkono PAA wamesisitiza kuwa eneo hilo pia lazima lijiinue kwa chochote lilicho nacho ili kufaidika katika serikali ijayo.
Wamesisitiza kuwa viongozi kutoka kanda hiyo lazima wazungumze kwa sauti moja ili kusukuma ajenda za eneo hilo.
Kulingana na PAA, Pwani imekosa mwelekeo ufaao kwa miaka mingi, lakini hilo lazima likomeshwe ili kufaidika katika serikali ijayo. Bw Maitha alisema kuhamishwa kwa shughuli kuu za bandari na biashara ya usafirishaji kutoka Mombasa hadi Nairobi na Naivasha kumeleta umaskini katika eneo hilo.
“Leo mzunguko wa pesa Mombasa umepungua kwa sababu maelfu ya kazi zimehamishwa kwingineko. Kazi hizi zilikuwa zikinufaisha kila mtu,” alisema.
Pia, viongozi hao wamelalamikia mkoa huo kutonufaika na maliasili zake licha ya kuchangia kwa kiasi kikubwa katika hazina ya kitaifa.
“Serikali iliingiza zaidi ya Sh12 bilioni kuweka mkakati wa maendeleo ya Uchumi wa Bahari lakini watu wa eneo hili wametengwa . Hiyo ina maana kwamba watu wa Pwani hawatakuwa popote kufikia wakati sekta hiyo itakapokamilika,” akasema Bw Maitha.
Viongozi hao walisikitika kuwa serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuwapa maskwota makazi mapya, kufufua viwanda mkoani humo kama ilivyoahidi katika Uchaguzi Mkuu wa 2013 na 2017.
“Haya yamechangia ukosefu wa ajira na matumizi ya dawa za kulevya. Lakini tunasema kwamba ni lazima tukomeshe hili. Wakati huu lazima tutie saini mkataba na mgombeaji ambaye atashughulikia masuala yetu,” alisema.
PAA hata hivyo imeshikilia kwamba itasimamisha wagombea kwa nyadhifa zilizosalia katika uchaguzi ujao.
Next article
Wamunyinyi kutoana kijasho na Wetang’ula kwa useneta